Prime
Mngqithi, Barker tofauti ipo hapa
MSIMU wa 2026-2027 unaelekea kuwa mmoja wa misimu yenye mvuto wa aina yake katika historia ya hivi karibuni ya Ligi Kuu ya NBC kutokana na vita ya kiufundi itakayowakutanisha makocha wawili kutoka Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi akiwa na Yanga na Steve Barker wa Simba.
Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, miamba hiyo miwili ya soka la Tanzania itaongozwa na makocha wenye asili moja, waliokulia katika mazingira ya soka la Afrika Kusini, lakini waliobeba falsafa tofauti kabisa za uchezeshaji. Hilo limeongeza hamasa kwa wadau wanaosubiri kuona ni mbinu zipi zitatawala msimu ujao.
Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ambaye pia amefanya kazi kwa miaka mingi Afrika Kusini na kuwafuatilia kwa karibu makocha hao wawili, anaamini ushindani wao unaweza kuufanya msimu huo kuwa darasa la mbinu na falsafa tofauti za soka.
“Makocha hawa nawafahamu vizuri. Wametokea mazingira yanayofanana, lakini kila mmoja amejijengea utambulisho wake. Hiyo ndiyo itakayofanya mechi zao ziwe za kipekee,” amesema Eymael.
Mngqithi anajiunga na Yanga akiwa na wasifu mzito baada ya kufanya kazi kwa zaidi ya miongo miwili katika soka la Afrika Kusini. Ametumikia klabu mbalimbali kama Golden Arrows na Chippa United, lakini jina lake liling’ara zaidi akiwa sehemu ya benchi la Mamelodi Sundowns.
Kwa upande wa Barker, anaingia katika msimu wake wa pili Simba akiwa tayari ameanza kujenga utambulisho wake. Kabla ya kutua Msimbazi Desemba 2025, alijijengea heshima kubwa akiwa kocha wa Stellenbosch FC, aliyoiongoza kutoka timu ya kawaida hadi kuwa moja ya klabu zenye ushindani mkubwa nchini Afrika Kusini, huku akitwaa Kombe la Carling Knockout na kuipeleka klabu hiyo kwenye mashindano ya CAF na kuishia robo fainali msimu wa 2024-2025 ilipotolewa na Simba kunako Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa Eymael, tofauti kubwa kati ya makocha hao inaanzia kwenye namna wanavyouona mchezo. Mngqithi ni kocha anayependa timu yake itawale mpira, ijenge mashambulizi kwa utulivu na kutumia pasi nyingi kuvunja safu ya mpinzani.
“Anapenda timu yake iwe na mpira zaidi. Huwajengea wachezaji utulivu wa kupishana pasi, kusogeza mpira hatua kwa hatua na kusubiri nafasi sahihi ya kuumiza mpinzani,” amesema Eymael.
Aliongeza kuwa, mara nyingi Mngqithi hutumia viungo wa kati kama injini ya timu, huku mabeki wakianza mashambulizi kutoka nyuma badala ya kutumia mipira mirefu. Mfumo huo huifanya timu yake kuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo kwa muda mrefu.
Kwa Barker, mtazamo ni tofauti. Eymael amesema kocha huyo hupendelea timu yake kuwa imara bila mpira lakini ikipata umiliki ibadilike haraka na kuwa tishio kwa mpinzani.
“Kwa ninavyomjua huwa hapotezi muda mwingi kwenye pasi nyingi. Akiona nafasi anaelekeza timu ishambulie moja kwa moja. Ni kocha anayependa uwiano mzuri kati ya kukaba na kushambulia,” amesema.
Tofauti ya kwanza ya kiufundi, kwa mujibu wa Eymael, ipo kwenye matumizi ya umiliki wa mpira. Mngqithi huamini mpira ndiyo silaha ya kwanza ya kujilinda na kushambulia, wakati Barker huamini kasi kutoka nyuma kwenda eneo la ushambuliaji ndiyo njia bora ya kuumiza wapinzani.
Tofauti ya pili ipo katika mfumo. Mngqithi hupendelea kukaba juu ili kuurejesha mpira haraka baada ya kuupoteza, jambo linalohitaji nidhamu kubwa ya kimfumo na utimamu wa mwili kwa wachezaji wake.
Kwa Barker namna yake ya kuweka presha kwa wapinzani huwa ya kimkakati zaidi. Mara nyingi timu yake hukaa katika umbo sahihi, humvutia mpinzani mbele kisha kutumia nafasi zinazoachwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza yenye kasi.
Katika usomaji wa mchezo, Eymael anaamini Mngqithi ni mmoja wa makocha wanaopenda kubadili maumbo ya timu katikati ya mchezo bila kupoteza utulivu wa mfumo. Barker naye hubadilika kulingana na mazingira ya mchezo lakini zaidi hulenga kuboresha uwiano wa safu ya ulinzi na ushambuliaji kuliko kubadili kabisa falsafa ya timu.
Kwa mtazamo wa Eymael, mashabiki wanaweza kuanza kuona tofauti hizo mapema kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 12, 2026 ambayo itakuwa kipimo cha kwanza cha falsafa mbili zinazotarajiwa kutawala mijadala ya soka.
Yanga imeamua kuweka kambi ya maandalizi Avic Town, Dar es Salaam ili kumpa Mngqithi muda wa kuingiza mfumo wake huku Simba ikitumia ushiriki wa Kombe la CECAFA Kagame nchini Rwanda kama fursa ya Barker kuendelea kuijenga timu yake kupitia mechi za ushindani.
Msimu uliopita, Barker aliweka msingi mzuri ndani ya Simba kwa kutwaa Kombe la Muungano na Kombe la CRDB, huku akiiongoza timu kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya NBC kwa tofauti ya pointi mbili pekee nyuma ya mabingwa Yanga.