Mikakati mipya ya Makata Polisi Tanzania
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Makata alisema licha ya mwenendo mzuri wa timu hiyo hadi sasa, ila bado wanahitaji kufanya vizuri zaidi, ili kuendana na ushindani uliopo na mlundikano wa ratiba za mechi wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea Oktoba 8, 2026.
WAKATI kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ikiendelea kwa sasa, kocha mkuu wa kikosi cha Polisi Tanzania, Mbwana Makata, amesema hawana muda wa mrefu zaidi kupumzika, isipokuwa wanaendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zijazo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makata alisema licha ya mwenendo mzuri wa timu hiyo hadi sasa, ila bado wanahitaji kufanya vizuri zaidi, ili kuendana na ushindani uliopo na mlundikano wa ratiba za mechi wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea Oktoba 8, 2026.
“Ni kweli tuna zaidi ya wiki mbili hadi tatu za kupumzika, ila kutokana na ushindani uliopo na ratiba kubana wakati tu Ligi Kuu itakaporudi, tunahitaji kujipanga na hali hilo ili kuendana na mazingira magumu mbele yetu,” alisema Makata.
Aidha, Makata alisema moja ya kazi kubwa anayoifanya kwa sasa ni kutengeneza balansi nzuri katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji, kwa sababu licha ya kasi kubwa ya kufunga mabao, ila bado wamekosa mwenendo mzuri wanaposhambuliwa.
“Uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa sio mzuri, hii sio picha nzuri kwa sababu kuna mechi unaweza ukafunga bao moja, ila ikiwa hutokuwa imara kulinda ni rahisi wapinzani kusawazisha, sasa hiyo ni kazi tunayoifanya kimkakati,” alisema.
Polisi iliyorejea Ligi Kuu msimu huu baada ya kushuka 2022-2023, imecheza mechi sita na kati ya hizo imeshinda tatu, sare moja na kupoteza mbili, ikishika nafasi ya tano na pointi zake 10, huku ikifunga mabao tisa na kuruhusu saba.
Makata ni miongoni mwa makocha wenye rekodi za kuvutia katika timu mbalimbali, ambapo mojawapo ni ya kuipandisha daraja Polisi Tanzania mara mbili kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara.