Mido yatua anga za Kagera Sugar
Muktasari:
- Milandu anayemudu kucheza nafasi ya kiungo wa kati kwa ufasaha, amefikia makubaliano ya awali kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho cha ‘Wanankurukumbi’ ambapo sasa zimebakia hatua chache kabla ya dili hilo la nyota huyo kukamilika rasmi.
BAADA ya Kagera Sugar kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, mabosi wa timu hiyo wanasuka upya kikosi hicho na sasa wako katika hatua za mwisho za kumsajili aliyekuwa kiungo mkabaji wa Dodoma Jiji, Daudi Milandu.
Milandu anayemudu kucheza nafasi ya kiungo wa kati kwa ufasaha, amefikia makubaliano ya awali kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho cha ‘Wanankurukumbi’ ambapo sasa zimebakia hatua chache kabla ya dili hilo la nyota huyo kukamilika rasmi.
Nyota huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji, Juni 15, 2024, akitokea Tabora United kwa sasa TRA United, amemaliza mkataba wake wa miaka miwili na kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, jambo ambalo limeipatia nguvu Kagera Sugar kuanza mazungumzo naye.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Samson Sikira amesema suala nzima la usajili limeanza tayari, japo utambulisho wa nyota wapya watakaokitumikia kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027, litaanza siku za hivi karibuni.
“Tumeingia kambini leo (jana Jumatatu) kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu, taratibu zote za usajili zimeshakamilika na tunachokisubiria ni kuwatambulisha, kwa sasa tuachane na tetesi ili tusubirie taarifa sahihi kwetu,” amesema Sikira.
Licha ya kauli ya Sikira, ila Mwanaspoti linatambua kiungo huyo amekamilisha usajili wa kujiunga na Kagera Sugar, ambapo anaungana na beki wa kulia, Dickson Mhilu aliyerejea tena ndani ya kikosi hicho kwa mara nyingine akitokea Dodoma Jiji.
Nyota wengine ni beki wa kushoto anayecheza pia beki wa kati, Boniface Onyango kutoka Kakamega Homeboyz, mshambuliaji, Collins Maina aliyetoka Fortune Sacco FC wote Wakenya na Naku Kazimoto anayecheza mshambuliaji kutokea Polisi Tanzania.