Mhilu mambo safi Geita Gold
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Bukombe uliopo mji mdogo wa Ushirombo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuisha kwa sare ya mabao 2-2, mshambuliaji huyo aliumia dakika ya 12 na kushindwa kuendelea kucheza.
MSHAMBULIAJI nyota wa Geita Gold, Yusuph Mhilu amepona vizuri majeraha yake ya nyama za paja aliyopata katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya timu hiyo dhidi ya Azam FC, iliyopigwa Agosti 28, 2026.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Bukombe uliopo mji mdogo wa Ushirombo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita na kuisha kwa sare ya mabao 2-2, mshambuliaji huyo aliumia dakika ya 12 na kushindwa kuendelea kucheza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mhilu alisema kwa sasa amepona kwa asilimia 100 na ameshajumuika na wachezaji wenzake ndani ya kikosi hicho kinachoendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi zijazo za Ligi Kuu Bara, baada ya kupisha kalenda ya FIFA. “Kwa sasa nimerejea katika hali yangu ya kawaida kutokana na majeraha ya nyama za paja niliyopata, awali niliumia tena baada ya kufosi kucheza mechi zilizofuatia, ila baada ya hapo niliamua kutulia kwanza ili nipone vizuri,” alisema Mhilu.
Aidha, Mhilu alisema kurejea kwake ni jambo nzuri kwa sababu kunaongeza wigo mpana wa machaguo kwa benchi lao la ufundi katika eneo la ushambuliaji, licha ya uwepo wa wachezaji wengine wengi na wazuri wanaocheza hata akiwa hayupo kikosini.
Mhilu aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwemo Yanga, Ndanda na Simba, alijiunga na Geita Gold, Julai 21, 2023, baada ya kuachana na Kagera Sugar, ambapo hadi sasa ameshaifungia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara kwa msimu huu wa 2026-2027. Mhilu anashika nafasi ya pili kwa wachezaji wa Geita Gold waliofunga mabao mengi ya Ligi Kuu Bara anayeongoza ni Mzambia Obrey Chirwa mwenye manne, akiendeleza kiwango bora tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea Kagera Sugar.
Chirwa aliyechezea Yanga, Azam FC, Namungo FC, Ihefu kwa sasa Singida Black Stars na KenGold FC kwa msimu wa 2025-2026, ndiye mfungaji bora wa Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 18 ambayo ni sawa na ya Maulid Shaaban wa Geita Gold.