Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mgunda ataja kinachoiangusha Namungo

Muktasari:

  • Namungo FC imeshacheza mechi saba za Ligi Kuu Bara, imepata ushindi mara mbili na kupoteza nne, jambo linaloifanya iwe na alama sita ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

KOCHA Juma Mgunda, amesema kutotumia vizuri nafasi wanazotengeneza kwenye safu ya ushambuliaji, pamoja na makosa ya eneo la ulinzi, ni miongoni mwa mambo makubwa yanayowagharimu na kuwafanya kupoteza pointi kwenye mechi zao.

Namungo FC imeshacheza mechi saba za Ligi Kuu Bara, imepata ushindi mara mbili na kupoteza nne, jambo linaloifanya iwe na alama sita ikiwa nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda alisema wamebaini upungufu huo na sasa wameanza kuangalia kwa kina ili kufanyia kazi, huku akisisitiza umuhimu wa wachezaji wake kuongeza umakini katika maeneo yote mawili.

“Tumeliona hilo, hasa kwenye kutumia nafasi ambazo tunazipata na pia makosa kwenye eneo la ulinzi. Haya ni mambo ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha yanarekebishika,” alisema Mgunda.

Kocha huyo alisema changamoto kubwa zaidi imekuwa ni baadhi ya makosa kujirudia mara kwa mara, hali ambayo imekuwa ikiwafanya kupoteza umakini katika nyakati muhimu za mchezo na hatimaye kuangusha pointi. “Makosa mengi yamekuwa yakijirudia sana. Tunapoteza umakini katika baadhi ya nyakati na mwisho wake tunajikuta tumeangusha pointi ambazo tulipaswa kuzichukua,”  alisema.

Mgunda aliongeza kuwa kwa sasa jambo kubwa ni kuhakikisha wachezaji wanaelewa maeneo ambayo wamekuwa wakikosea na kuyafanyia kazi katika mazoezi ili timu iwe na umakini zaidi kwenye mechi zijazo.

“Kikosi chetu hakiwezi kumudu kuendelea kupoteza pointi kutokana na makosa ambayo yanaweza kurekebishwa, hivyo nidhamu na umakini zaidi katika safu ya ushambuliaji na ulinzi unahitajika.”

Mechi ijayo ya Namungo FC itakuwa dhidi ya TRA United, mchezo huo ulipangwa kuchezwa Oktoba 8, 2026 kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa, Lindi.