Mgombea ujumbe Yanga ajiondoa dakika za mwisho
Muktasari:
- Kihinga, ambaye alikuwa mjumbe aliyeteuliwa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, katika Kamati ya Utendaji iliyopita, alikuwa miongoni mwa wagombea 16 waliokuwa wakiwania nafasi hizo, lakini akaamua kujiondoa bila sababu zake kuwekwa wazi.
Mchakato wa uchaguzi wa Kamati ya Utendaji ya Yanga umepata mabadiliko ya ghafla baada ya mmoja wa wagombea, Gerrard Kihinga, kujiondoa dakika za mwisho kabla ya upigaji kura kuanza.
Kihinga, ambaye alikuwa mjumbe aliyeteuliwa na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, katika Kamati ya Utendaji iliyopita, alikuwa miongoni mwa wagombea 16 waliokuwa wakiwania nafasi hizo, lakini akaamua kujiondoa bila sababu zake kuwekwa wazi.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi unaofanyika kwenye Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Yanga, Malangwe Mchungahela, alisema mmoja wa wagombea amejiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.
"Tulikuwa na wagombea 16, lakini mmoja wao amejiondoa," alisema Mchungahela bila kulitaja jina la mgombea huyo.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwanaspoti umebaini kuwa aliyejiondoa ni Gerrard Kihinga, baada ya jina lake kutokutajwa miongoni mwa wagombea waliopewa nafasi ya kujinadi na kuomba kura mbele ya wanachama 877 waliohudhuria mkutano huo.
Baada ya kujiondoa kwa Kihinga, idadi ya wagombea imebaki 15.
Miongoni mwa wanaotetea nafasi zao ni Alexander Ngai, Rodgers Gumbo, Yanga Makaga, Munir Said Seleman na Seif Gulamali.
Wagombea wengine wanaowania nafasi hizo ni Injinia Mustapha Himba, Prisca Kishamba, Julius Koyi, Saady Khimji, Freddy Mahembe, Mshindo Hamza Msola, Issa Mangungu, Farid Afif, Mohammed Mwenda na Mzee Mwinyi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, wanachama watawachagua wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji, huku wajumbe wawili wakiteuliwa na Rais wa klabu.