Messi aibuka kwa mara ya kwanza Barcelona
Muktasari:
- KATIKA toleo lililopita mwandishi, Luca Caioli alielezea namna Ronaldo alivyopewa jezi namba 7 akaogopa na kuitaka namba 28 lakini Ferguson akasisitiza apewe namba 7. Sasa endelea…
KATIKA toleo lililopita mwandishi, Luca Caioli alielezea namna Ronaldo alivyopewa jezi namba 7 akaogopa na kuitaka namba 28 lakini Ferguson akasisitiza apewe namba 7. Sasa endelea…
Lakini huo ulikuwa mwanzo tu wa msimu mrefu, msimu ambao atatakiwa kuuzoea na kuendana na aina ya uchezaji wa kutumia nguvu, msimu ambao Man United iliumaliza vibaya kwa kumaliza ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Chelsea na Arsenal na taji pekee walilobeba msimu huo ni lile la FA.
Katika fainali hiyo ya FA Man United iliumana na Millwall na Ronaldo akafunga moja ya mabao matatu ya ushindi ya timu hiyo na akawa mtu muhimu katika safu ya ushambuliaji na ingawa hakuwa nyota wa mchezo lakini kila mtu alikuwa akimzungumzia.
Alimaliza msimu wake wa kwanza akiwa katika kiwango cha juu, alifunga jumla ya mabao manane katika mechi 39 alizocheza katika mashindano yote ya msimu huo.
Pia alipata kura 10,000 za mashabiki wa Man United na hatimaye akatwaa tuzo ya Sir Matt Busby ya mwanasoka bora wa mwaka wa klabu hiyo.
Msimu huo huo mchezaji mwingine kinda akaibuka na kuianza safari yake ya kusaka mafanikio katika soka la kiwango cha juu.
Siku ya Novemba 16, 2003 itaendelea kubaki milele katika kumbukumbu za Lionel Messi, ndio kwanza alikuwa na miaka 16 na miezi minne na siku 23 alipoingia uwanjani akiwa katika kikosi cha kwanza cha Barcelona kwa m ara ya kwanza.
Siku hiyo walikuwa wakicheza mechi ya kirafiki na FC Porto ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa Uwanja wa Dragao. Messi aliingia katika dakika ya 74 na kucheza kwa dakika 15 zilizobaki ambako alitengeneza nafasi mbili za mabao.
Msimu wa 2004/05
Kabla hata mwaka mmoja haujaisha, Oktoba 26, 2004 Messi alicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani na kuwa mchezaji mwenye umri mdogo katika historia ya Barca kucheza katika Ligi Kuu Hispania yaani La Liga (rekodi ambayo baadaye ilivunjwa na Bojan Krkic).
Hata hivyo, alilazimika kusubiri hadi Mei Mosi 2005 kabla ya kufunga bao lake la kwanza, bao hilo alilifunga katika dakika ya 34 katika mechi ya La Liga, ubao wa matangazo ulisomeka 1-0, Barca walikuwa mbele dhidi ya Albacete.
Kocha Frank Rijkaard alimtoa Samuel Eto’o na kumuingiza Messi na kumpanga Messi katika eneo ambalo halikuwa la kawaida, eneo la mshambuliaji wa kati.
Messi aliitumia vizuri pasi ya Ronaldinho na kuudokoa mpira ambao ulimpita kwa juu kipa na kujaa wavuni, hapo ilikuwa ni ni kama miezi miwili hivi kabla ya kusherehekea kutimiza umri wa miaka 18.
Si hili tu lakini pia siku hiyo akaweka historia ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo kupata bao katika La Liga (rekodi nyingine ambayo ilivunjwa na Krkic Oktoba 20, 2007 alipofunga bao katika mechi dhidi ya Villareal).
Kwa upande mwingine haukuwa msimu uliochangamka kwa Ronaldo, ilimchukua hadi Desemba 5, 2004 kupata bao lake la kwanza katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Southampton.
“Alikuwa ndio kwanza ametuahidi mabao 12 na tunatumaini huo ndio mwanza,’’ alisema Ferguson. Hata hivyo Ronaldo alichoweza ni mabao tisa katika mechi 50. Pia huo haukuwa msimu mzuri kwa United ambao walimaliza bila taji huku Chelsea wakibeba taji la Ligi Kuu England.
Itaendelea Jumamosi ijayo…