Mayele aitaja Yanga CAF
Muktasari:
- Mayele amesema Yanga ikijipanga vizuri inaweza kwenda mbali katika michuano hiyo, akitaja kutokuwepo kwa baadhi ya vigogo wa soka la Afrika kama Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns kuwa ni nafasi nyingine kwa timu hiyo kupambana kutimiza malengo yake.
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele ambaye kwa sasa anaichezea Al Ahly Tripoli ya Libya, amesema Yanga ina nafasi kubwa ya kufika hatua za juu katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, akiamini kikosi hicho kina ubora wa kufanya vizuri.
Mayele amesema Yanga ikijipanga vizuri inaweza kwenda mbali katika michuano hiyo, akitaja kutokuwepo kwa baadhi ya vigogo wa soka la Afrika kama Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns kuwa ni nafasi nyingine kwa timu hiyo kupambana kutimiza malengo yake.
“Kwa mfano ukiangalia Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, ukitoa Pyramids, hakuna timu ambayo watu wanaiona moja kwa moja kuwa inaweza kufika fainali. Yanga ina nafasi kubwa, wakijipanga vizuri wanaweza kwenda mbali kwa sababu hakuna Al Ahly ya Misri wala Mamelodi Sundowns,” alisema Mayele.
Akizungumzia ushindi wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya Azam FC katika mchezo wa ufunguzi wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Mayele amesema haikuwa mechi rahisi kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao anawafahamu vizuri.
Amesema walijua Azam ingeanza kwa presha kubwa, hivyo waliamua kuwashambulia mapema na kuwazuia wasiwe na nafasi nzuri ya kuanzisha mashambulizi yao, mpango ambao uliwasaidia kupata mabao mawili kabla ya wenyeji kurejea kwa bao moja.
“Mechi ilikuwa ngumu kwa sababu Azam ina wachezaji wazuri na mimi nawafahamu karibu wote. Tulijua wataweka presha dakika za mwanzo, hivyo tulitaka kuwashambulia kule kwao ili wapate shida kutoka na mpira. Tulifanikiwa kupata bao la kwanza, kisha la pili likafuata,” alisema.
Mayele ameongeza kuwa Azam iliwapa wakati mgumu baada ya kufanya mabadiliko kipindi cha pili, hasa baada ya mshambuliaji wa timu hiyo kuingia na kuanza kuwasumbua, lakini walibadilisha namna ya kumkaba ili kumzuia asigeuke na kuelekea langoni.
Amesema ushindi huo ulikuwa muhimu kwa Al Ahly Tripoli kwa sababu wameanza michuano hiyo kwa kupata pointi tatu ugenini, lakini hawatakiwi kubweteka kwa kuwa bado wana michezo migumu mbele yao.
Ameeleza kuwa klabu hiyo imewekeza katika kusajili wachezaji wenye majina na ubora mkubwa, hivyo matarajio ya mashabiki wa Libya ni kuona timu hiyo inafanya vizuri katika michuano ya Afrika.
Mayele pia amezungumzia nafasi ya Simba na Singida Black Stars katika michuano ya Afrika, akizitaka timu hizo kuendelea kupambana na kila mchezaji kutimiza wajibu wake ili kuzipeleka mbele timu hizo.
Kuhusu kiwango chake binafsi baada ya kushindwa kufunga dhidi ya Azam, Mayele amesema hana presha kwa sababu katika soka kufunga na kutofunga ni sehemu ya mchezo, akisisitiza kuwa anamshukuru Mungu kwa kila jambo.