Mayanga awajia juu mastaa Mbeya City
Muktasari:
- Mbeya City FC kwa sasa ina pointi 10 baada ya kupoteza michezo mitatu msimu huu, ambapo katika uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine wamecheza michezo minne na kupata matokeo mchanganyiko ya ushindi mara mbili dhidi ya Dodoma Jiji na Mashujaa FC, pamoja na vipigo viwili dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar.
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amewajia juu wachezaji wake baada ya kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar, huku akisema makosa ya umakini ndiyo yaliyowagharimu.
Mbeya City FC kwa sasa ina pointi 10 baada ya kupoteza michezo mitatu msimu huu, ambapo katika uwanja wao wa nyumbani wa Sokoine wamecheza michezo minne na kupata matokeo mchanganyiko ya ushindi mara mbili dhidi ya Dodoma Jiji na Mashujaa FC, pamoja na vipigo viwili dhidi ya Geita Gold na Kagera Sugar.
Akizungumza na Mwanaposti, Mayanga amesema wachezaji wake walishindwa kutekeleza majukumu yao kwa umakini, hasa katika safu ya ulinzi na eneo la ushambuliaji, hali iliyowapa wapinzani nafasi ya kupata ushindi muhimu ugenini.
“Wachezaji walifanya makosa makubwa ya umakini ambayo yametugharimu kupoteza mchezo huu. Tulikuwa na mapungufu kwenye ulinzi na hata mbele tulishindwa kutumia nafasi tulizopata,” amesema Mayanga.
Katika mchezo huo, Kagera Sugar ndiyo ilianza kupata bao kupitia Emmanuel Mvuyekule dakika ya 37, lakini Mbeya City ilisawazisha dakika ya 43 kupitia Hassan Hajji ‘Cheda’, na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Kipindi cha pili, Kagera Sugar ilirejea kwa kasi na Mudathir Said kufunga mabao mawili dakika ya 58 na 73, na kuipa timu hiyo ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo ambao wenyeji walishindwa kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao.
Kipigo hicho ni pigo kwa Mayanga, aliyerejea rasmi Mbeya City Aprili 2026 akitokea Mashujaa FC, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Mecky Maxime. Kocha huyo sasa analazimika kurekebisha makosa ya kikosi chake ili kurejesha ushindani katika michezo inayofuata.