Mayanga ataka mechi za kirafiki
Muktasari:
- Mayanga hajavunja kambi ya timu hiyo, akisema anataka kutumia wiki hizi za mapumziko kurekebisha upungufu uliojitokeza katika mechi sita za kwanza za msimu wa 2026-2027.
MBEYA City inataka kupata mechi mbili za kirafiki, huku kocha Salum Mayanga akilenga kuzitumia kuimarisha kikosi chake baada ya kukosa muda wa kutosha wa maandalizi kabla ya msimu kuanza.
Mayanga hajavunja kambi ya timu hiyo, akisema anataka kutumia wiki hizi za mapumziko kurekebisha upungufu uliojitokeza katika mechi sita za kwanza za msimu wa 2026-2027.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema changamoto alizoziona kwenye mechi hizo zitafanyiwa kazi kuanzia safu ya ulinzi, eneo la kiungo hadi ushambuliaji ili kuifanya timu iwe imara zaidi.
“Hatukupata muda wa kutosha kwenye pre-season, hivyo nimeamua kutumia kipindi hiki kuimarisha timu na kufanyia kazi mapungufu tuliyoyaona kwenye mechi sita za kwanza,” alisema Mayanga.
Kocha huyo alisema anahitaji pia mechi za kirafiki ili kupima maboresho anayoyafanya na kuwaweka sawa wachezaji wake kabla ya kurejea kwenye mashindano. “Tunataka kucheza mechi mbili za kirafiki katika kipindi hiki ili kujiweka sawa na kuona maeneo ambayo bado yanahitaji maboresho,” alisema.
Mbeya City sasa inaendelea na maandalizi hayo ikilenga kurejea kwenye Ligi Kuu Bara, ikiwa na kikosi kilichoboreshwa, huku mechi hizo mbili za kirafiki zikiwa sehemu ya maandalizi yake. Mbeya City imecheza mechi sita ikiwa rekodi ya kushinda tatu, sare moja na kupoteza mbili, ikifikisha pointi 10, imefunga mabao sita na kufungwa manne.