Matokeo ZPL yamshtua kocha Polisi
Muktasari:
- Timu hiyo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikicheza mechi tano, kati ya hizo imeshinda mbili na sare tatu, haijapoteza ikikusanya pointi tisa.
UNAWEZA kusema ni kama hivi sasa timu ya Polisi imeanza kukata moto baada ya kutoka sare mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), huku matokeo hayo yakionekana kumshtua kocha msaidizi wa kikosi hicho, Awesu Maulid.
Katika sare hizo tatu, Polisi imeshindwa kufungana dhidi ya Mafunzo na Mwenge, huku ikitoka 1-1 dhidi ya Zimamoto. Kabla ya hapo, ilianza kwa kuichapa KVZ bao 1-0, kisha ikaipiga Mlandege 2-0.
Akizungumzia mwenendo huo, Awesu amesema amekubaliana na matokeo hayo kwani ndio mpira ulivyo, lakini si mazuri upande wao, hivyo watajipanga kwa mechi zijazo kufanya vizuri.
Amesema bado ana imani na timu hiyo kwa sababu wachezaji wanapambana kupata matokeo mazuri ingawa kuna maeneo wanazidiwa.
Amesema baada ya kuanza vizuri, anajua kwa sasa timu zinajipanga vyema lakini hilo halitozuia kushindwa kutimiza malengo waliyonayo.
"Mpira lazima ukubaliane na mtokeo ya aina zote, hivyo na mimi nimeyapokea, nitarekebisha makosa yaliyojitokeza," amesema.
Mbali na hilo, kocha huyo amewasihi waamuzi kuchezesha mpira kwa kufuata sheria kwa lengo la kuongeza ushindani wa ligi hiyo.
Timu hiyo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikicheza mechi tano, kati ya hizo imeshinda mbili na sare tatu, haijapoteza ikikusanya pointi tisa.