Mastaa Man United wamtaka Ferguson kumsajili Ronaldo
Muktasari:
- TOLEO lililopita mwandishi, Luca Caioli alizungumzia maisha ya Ronaldo katika klabu ya Sporting na jinsi timu hiyo ilivyomaliza vibaya msimu wa 2002/03 ingawa kwa Ronaldo kipaji chake kilianza kuonekana na kutoa dalili njema. Endelea…
TOLEO lililopita mwandishi, Luca Caioli alizungumzia maisha ya Ronaldo katika klabu ya Sporting na jinsi timu hiyo ilivyomaliza vibaya msimu wa 2002/03 ingawa kwa Ronaldo kipaji chake kilianza kuonekana na kutoa dalili njema. Endelea…
Walimaliza ligi wakiwa nafasi ya tatu wakiwa nyuma kwa pointi 27 dhidi ya vinara FC Porto wakati huo wakinolewa na Jose Mourinho na pointi 16 nyuma ya Benfica ambao walishika nafasi ya pili.
Msimu huo ukawa kama mwanzo wa kunawa mikono au majanga kwa klabu hiyo, lakini kwa Ronaldo haikuwa hivyo, kwake ikawa kama mabadiliko ya maisha kutoka hatua moja kwenda nyingine.
Safari yake ya kuelekea Man United bado kidogo ishindikane, kwa muda mrefu United walikuwa katika mazungumzo na Sporting. Akademi ya Sporting ilikuwa kama sehemu ya Man United, walikuwa ndio chaguo la kwanza kwa mchezaji yeyote chipukizi aliyeonekana kuwa na kipaji.
Na ilikuwa kama jambo la lazima kwa Sporting kuwaarifu kuhusu mchezaji yeyote aliyekuwa kivutio, pamoja na yote hayo mazungumzo yao ilikuwa siri kubwa.
Hakuna aliyekuwa tayari kutoa habari hiyo nje hadi wakati wa mechi ya kirafiki baina ya timu hizo ambayo pia ilikuwa ya Lisbon kuzindua uwanja wao mpya.
Hiyo ilikuwa Agosti 6, 2003, ndiyo siku ambayo Ronaldo aliingia uwanjani kuwaonyesha mashabiki wa Man United kile anachoweza kuwafanyia, mgongoni alikuwa na jezi namba 28, na hiyo ilikuwa mechi yake bora na Sporting.
Alianza vizuri na kuwaweka katika wakati mgumu mabeki wa Man United kwa namna alivyokuwa akipepea kwenye wingi, alimjaribu kipa wa Man United, Fabien Barthez kwa shuti la mbali na jingine la karibu, yote hayo Barthez, kipa Mfaransa alionyesha ubora wake kwa kuyaokoa.
Katika dakika ya 25 alimshirikisha vizuri Felipe ambaye hatimaye aliifungia Sporting bao la kwanza, ukiachana na juhudi hizo kwa ujumla, Ronaldo alionyesha umahiri katika kupiga chenga, kukwepa madaluga, kukimbia kwa kasi na mengi mengine.
Baada ya hapo wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kila mmoja, wachezaji wote mastaa walikuwa wakimwambia kocha wa wakati huo, Sir Alex Ferguson amsajili staa huyu wa Ureno (Ronaldo).
Pamoja na wachezaji kutoa kauli hizo lakini Ferguson akabaki kimya, hakuwa na nia ya kutangaza kwa wachezaji wake kwamba tayari mpango mzima ulishakamilika.
Ferguson alitumia ujanja, alichotaka ni kuona kinda wake huyo (Ronaldo) anakubalika kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuanzia siku ya kwanza na njia ipi ingekuwa sahihi zaidi ya kuwaacha wachezaji wenyewe wafikirie kwamba wana kitu cha kufanya ili kumtoa mchezaji huyo Sporting Lisbon.
Wiki moja baada ya mechi hiyo ya kirafiki iliyoisha kwa Sporting kuichapa Man United mabao 3-1, Ronaldo aliwasili Man United kwa ajili ya kukutana na Ferguson, aliamini kwamba angesaini mkataba, angefanyiwa vipimo vya afya.
Pia angetembelea Old Trafford na kuangalia mazingira na vitendea kazi na baada ya hapo angerudi Lisbon na kubaki katika klabu hiyo kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Hata hivyo, Ferguson alikuwa na mpango mwingine, mara baada ya kuwasili na kusaini mkataba (wa Euro 2 milioni mwa mwaka zaidi ya Euro 150,000 kwa mwezi ukilinganisha na Euro 2,000 alizokuwa akizipata Lisbon). Ferguson akakaa na wakala wa Ronaldo, Jorge Mendes.
“Sina ninachojua katika Kiingereza,” Ronaldo anakumbukwa kuliambia gazeti la Publico la Ureno miaka kadhaa baadaye. “Mendes alinieleza kwamba Ferguson anataka nibaki Manchester, nilishituka na kujawa na wasiwasi.”
Hakujua afanye nini, hata vitu vyake hakuwa amevibeba, alitakiwa aanze mazoezi Carrington na baadaye angerudi kuchukua vitu vyake.
Itaendelea Jumamosi ijayo…