Masalanga: Nimejifunza kuwa na subira
Muktasari:
- Masalanga, aliyejiunga na Yanga msimu uliopita katika dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black Stars, amesema anaendelea kupambana na kuamini kuwa siku moja atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake.
KIPA wa Yanga, Hussein Masalanga, amesema hatakata tamaa licha ya ushindani mkubwa ndani ya kikosi hicho, akiamini kuwa bidii na kujituma mazoezini vitamwezesha kupata nafasi katika kikosi hicho.
Masalanga, aliyejiunga na Yanga msimu uliopita katika dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black Stars, amesema anaendelea kupambana na kuamini kuwa siku moja atapata nafasi ya kuonyesha uwezo wake na kuisaidia timu hiyo kufikia malengo yake.
“Ni msimu mzuri unaohitaji mapambano makubwa. Kazi yangu ni soka, hivyo lazima niendelee kupambana na kufanya mazoezi. Ninaamini kuna siku huduma yangu itakuwa na msaada ndani ya timu, na ndiyo maana nilisajiliwa,” amesema Masalanga.
Ameongeza kuwa amejifunza kuwa na subira katika nyakati za mafanikio na changamoto, jambo linalomsaidia kuendelea kupambana bila kukata tamaa.
“Nimejifunza kumshukuru Mungu wakati wa mafanikio na hata nyakati ambazo mambo yanakuwa magumu au ninapokosa nafasi ya kucheza. Ndiyo maana sijawahi kukata tamaa, bali ninaendelea kuipambania kesho yangu njema,” amesema.
Akizungumzia ushindani wa makipa ndani ya Yanga, Masalanga amesema unampa nafasi ya kujifunza na kujiimarisha zaidi, akiwataja Djigui Diarra na Mshery kuwa miongoni mwa makipa wenye uwezo mkubwa.
Amesema anafurahia ushindani huo kwa kuwa unamsaidia kuboresha uwezo wake na kuongeza maarifa ya mchezo.
“Makipa waliopo Yanga ni wazuri na wenye uwezo mkubwa. Napenda ushindani ambao utanijenga na kunifanya kuwa bora zaidi. Kwa mfano, Diarra ni kipa wa kisasa aliyekamilika katika maeneo mengi, kama ilivyo kwa Mshery,” amesema.
Kuhusu nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Masalanga amesema uamuzi wa kuchagua wachezaji unabaki kwa makocha, lakini yeye ana ndoto ya kuendelea kulitumikia taifa kupitia soka.
“Makocha ndiyo wanaojua ni mchezaji gani wa kumtumia na wakati gani. Wachezaji tupo wengi, lakini binafsi natamani kila wanapochaguliwa wachezaji wa timu ya taifa, na mimi niwemo ili niendelee kulitumikia taifa langu kupitia mpira wa miguu,” amesema.