Mao Zedong yakusanya milioni 47.4
JUMLA ya Sh47.4 milioni zimekusanywa kutokana na shughuli mbalimbali zilizofanyika katika Uwanja wa Mao Zedong, Zanzibar katika miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Baraza la Jiji Zanzibar kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2026/2027, Mwenyekiti wa baraza hilo, Salmin Amour Abdalla amesema makusanyo hayo yametokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa baada ya Serikali kulikabidhi baraza jukumu la kusimamia uwanja huo.
Taarifa hiyo iliwasilishwa katika ukumbi wa mikutano wa Michenzani Mall, mjini Unguja na Salmin amesema miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuimarisha mifumo ya usimamizi, kushirikisha sekta binafsi katika huduma za usafi na usimamizi wa maegesho, pamoja na kutumia mfumo wa kisasa wa uendeshaji.
Amesema baraza hilo linaendelea kuwasiliana na Wizara ya Fedha ili kupata idhini ya kutumia mapato yanayokusanywa katika uwanja huo kugharimia huduma za usafi, umeme na matengenezo ya miundombinu.
“Idhini hiyo ikipatikana, fedha hizo zitasaidia kugharamia huduma za usafi, umeme na matengenezo ya miundombinu,” amesema.
Alifafanua hatua hiyo inalenga kuufanya uwanja huo kuwa na mazingira bora, kutoa huduma nzuri kwa watumiaji na kuwa chanzo endelevu cha mapato kwa Baraza la Jiji Zanzibar. Kwa sasa, Uwanja wa Mao Zedong unasimamiwa na Baraza la Jiji Zanzibar baada ya kuingia mkataba wa miaka mitatu na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar.