Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Manzoki kama Mzize, Vipers yamlinda

Muktasari:

  • Manzoki, ambaye kwa muda mrefu aliwahi kuhusishwa na usajili wa Simba, amerejea Vipers dirisha hili la usajili akitokea Eastern District ya Ligi Kuu ya Hong Kong.

WAKATI mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, akianza kurejea taratibu kikosini baada ya kuuguza majeraha, hali kama hiyo ndiyo inayomkabili mshambuliaji wa Vipers SC ya Uganda, Cesar Lobi Manzoki.

Manzoki, ambaye kwa muda mrefu aliwahi kuhusishwa na usajili wa Simba, amerejea Vipers dirisha hili la usajili akitokea Eastern District ya Ligi Kuu ya Hong Kong.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa DR Congo alirejea akiwa na majeraha yaliyomuweka nje ya programu kamili ya maandalizi ya msimu mpya.

Kutokana na hali hiyo, benchi la ufundi la Vipers linaloongozwa na Denis Lavagne limeamua kutomharakisha kurejea uwanjani, likimlinda katika mechi za mwanzo za Kombe la CECAFA Kagame ili kumpa muda wa kuendelea na matibabu pamoja na mazoezi maalumu ya kurejesha utimamu wake.

Hatua hiyo inafanana na ilivyo kwa Mzize wa Yanga ambaye naye amekuwa akirejeshwa taratibu baada ya kuuguza majeraha huku benchi la ufundi likiepuka kumuingiza kwenye ushindani mkali kabla hajawa tayari.

Licha ya kutokuwa na huduma ya Manzoki, Vipers imeonyesha ubora mkubwa kwenye michuano ya CECAFA Kagame na tayari imekata tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali ikiwa bado ina mchezo mmoja wa hatua ya makundi. Mabingwa hao wa Uganda walijihakikishia nafasi hiyo baada ya kushinda mechi zao mbili za kwanza za Kundi A, wakianza kwa kuichapa Garde, kabla ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya na kufikisha pointi sita zilizowahakikishia nafasi ya kumaliza miongoni mwa timu bora za kundi hilo.

Baada ya kufuzu mapema, Vipers ilishuka dimbani jana kumalizia ratiba ya makundi kwa kuivaa APR ya Rwanda katika mchezo uliokuwa na umuhimu wa kuwania uongozi wa kundi na kuongeza morali kuelekea hatua ya mtoano.