Kocha Kenya aiangukia FKF
Muktasari:
- Selebwa amekutana na changamoto kubwa wakati wa kuunda kikosi kitakachoshiriki michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (U-20 AFCON), inayofanyika Tanzania, baada ya wachezaji wengi waliowakilisha Kenya katika fainali zilizopita za U-20 AFCON nchini Misri kutokuwa na sifa ya kushiriki tena kutokana na umri.
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Kenya chini ya miaka 20, Rising Stars, Gilbert Selebwa, ametoa wito kwa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na Serikali kupanga mapema na kuboresha utunzaji wa nyaraka za wachezaji ili kuepusha changamoto za dakika za mwisho wakati wa kuunda kikosi cha mashindano makubwa ya vijana.
Selebwa amekutana na changamoto kubwa wakati wa kuunda kikosi kitakachoshiriki michuano ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 (U-20 AFCON), inayofanyika Tanzania, baada ya wachezaji wengi waliowakilisha Kenya katika fainali zilizopita za U-20 AFCON nchini Misri kutokuwa na sifa ya kushiriki tena kutokana na umri.
Zaidi ya wachezaji 70 walipitia katika mchakato wa usaili, lakini baadhi yao walishindwa kuingia kwenye kikosi cha mwisho kutokana na kuwa na umri mkubwa au kutokuwa na hati halali za kusafiria ambazo zingeweza kukamilishwa kwa wakati kabla ya mashindano hayo yanayofanyika kuanza Sptemba 15 hadi 25 jijini Dar es Salaam.
Hali hiyo ilimlazimisha kocha huyo kugeukia mashindano ya kitaifa ya shule yanayosimamiwa na Kenya Secondary School Sports Association (KSSSA), ambako benchi la ufundi liligundua vipaji kadhaa vilivyofanikiwa kupata nafasi katika kikosi cha wachezaji 25.
Wachezaji saba kutoka shule mbalimbali wamejumuishwa kwenye kikosi hicho akiwemo Theodore Mwangi wa Ongata Academy, Eugene Bellety, Julius Ochieng ‘Agwambo’, Brighton Nacheri wa Kakamega School; Brighton Omondi na Stephen Ouma wa St. Mary’s Yala.