Manqoba v Barker, Dabi ya FVS
Muktasari:
- Simba na Yanga zimeanza kwa kishindo msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila moja ikishinda mechi zake zote tano za mwanzo.
KOCHA wa Simba, Steve Barker na mwenzake wa Yanga, Manqoba Mngqithi watakutana ana kwa ana leo Jumamosi jioni, kila mmoja akilenga kuipa timu yake ushindi katika Dabi ya Kariakoo inayosubiriwa kwa hamu.
Simba na Yanga zimeanza kwa kishindo msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kila moja ikishinda mechi zake zote tano za mwanzo.
Rekodi hizo nzuri zitawekwa rehani zitakapokutana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kuanzia Saa 1:00 usiku leo.
Mbali na ushindani wa vikosi hivyo, imethibitishwa kuwa mfumo wa usaidizi wa video kwa waamuzi (FVS) utatumika katika mchezo huo. Teknolojia hiyo ilitumika hivi karibuni katika michuano ya COSAFA ya vijana wenye umri chini ya miaka 20.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Mngqithi amesema wamefanya uchambuzi wa kina wa kikosi cha Simba ili kubaini uwezo na udhaifu wake kabla ya dabi hiyo.
“Tulitumia takribani wiki mbili tangu mapumziko hadi sasa kuboresha mbinu zetu, huku tukiiheshimu Simba na kuikabili kwa unyenyekevu kwa sababu ni timu kubwa,” Mngqithi alinukuliwa na Pan Africa Football.
“Tuliangalia nguvu na udhaifu wao, tukachambua uwezo wa kila mchezaji na kumtathmini mmoja baada ya mwingine wale tunaowaona wanaweza kutuletea madhara.
“Baadaye tulishirikisha taarifa hizo na wachezaji wengine wa timu yetu ili kila mmoja aelewe changamoto tunayoweza kukutana nayo.”