Maniche atoa hofu mashabiki Mtibwa Sugar
Muktasari:
- Katika mechi nne ilizocheza Mtibwa Sugar kabla ya jana ugenini dhidi ya IAA SC ya jijini, Arusha, imeshinda mbili, sare moja na kupoteza pia moja, ikiwa nafasi ya sita na pointi saba, huku ikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu matatu.
KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’ amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwaunga mkono kama kawaida, licha ya kuingiwa na hofu zaidi, baada ya wachezaji wengi wa kikosi hicho kuondoka na kujiunga na klabu mbalimbali za Ligi Kuu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maniche amesema mpira wa miguu ni ajira na mchezaji ni kazi yake anayoitegemea kwa ajili ya kujipatia kipato, hivyo, inapotokea fursa nzuri sehemu nyingine ni ngumu kumzuia, jambo ambalo ni la kawaida kwa sasa.
“Ninachowaomba mashabiki zetu waendelee kuonyesha sapoti yao ili tutimize malengo ya kuirudisha tena Mtibwa Sugar Ligi Kuu, sio muda wa kuangalia ya nyuma, isipokuwa tunapambana kutengeneza kikosi imara na cha ushindani,” amesema Maniche.
Maniche aliyeipandisha daraja Mtibwa Sugar kutoka Championship hadi Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, kisha kushuka tena msimu wa 2025-2026, ilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 27, amesema mwenendo wa timu hiyo sio mbaya na unawapa matumaini.
Katika mechi nne ilizocheza Mtibwa Sugar kabla ya jana ugenini dhidi ya IAA SC ya jijini, Arusha, imeshinda mbili, sare moja na kupoteza pia moja, ikiwa nafasi ya sita na pointi saba, huku ikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu matatu.