Malota asimulia kilichoiponza Simba Fainali CAF 1993
Muktasari:
Malota anasema miaka ya nyuma klabu ya Simba ilikuwa na matukio mengi, msimu haukupita bila tukio la kimgogoro kwa viongozi likiwamo la mwaka 1987 ambapo wachezaji walitakiwa wachague kati ya wazee na uongozi chini ya David Ngonya.
Dar es Salaam. Mwaka 1993 utabaki katika orodha ya matukio mabaya kwa klabu ya Simba, baada ya kukosa ubingwa wa Kombe la CAF
Kitendo cha Simba kutotwaa Kombe la CAF baada ya kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast katika ardhi yake ya Tanzania kinawauma mashabiki wa klabu hiyo mpaka sasa.
Timu hiyo ilishindwa kutwaa ubingwa katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru), Novemba 26, 1993.
Hatua ya Simba kukosa ubingwa mbele ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, iliibua mjadala kila kona na baadhi ya wadau walidai ni hujuma.
Wapo waliodai baadhi ya wachezaji walicheza mchezo mchafu kwa kushirikiana na viongozi wa wakati huo waliokosa uadilifu.
Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo Malota Soma alikuwepo katika kikosi cha Simba kilichocheza mchezo huo wa fainali.
Malota anaeleza kilichotokea hadi wakakosa ubingwa licha ya kuahidiwa zawadi ya kila mchezaji kupewa gari na aliyekuwa mfadhili mkuu wa klabu hiyo Azim Dewji.
Malota anasema hakuna hujuma iliyofanyika katika mchezo ule tofauti na madai ya baadhi ya wadau wakiwemo mashabiki wa klabu hiyo wanaodai kuna mchezo mchafu ulifanyika.
Simba iliweka kambi Zanzibar kujiandaa kwa mchezo na kila mchezaji alikuwa amejiandaa kucheza kwa nguvu ili kutwaa ubingwa.
“Chanzo cha sisi kufungwa na Stella ni viongozi, walitupa presha kubwa. Tulikuwa hatulali mara ameingia kiongozi wa Serikali amesema hivi, hatujakaa sawa ameingia mwingine. Maandalizi hatukufanya kwa kiwango bora akili za viongozi ilikuwa kuandaa sherehe za ubingwa.
“Mdhamini wa Simba wakati huo, Azim Dewji alituahidi gari aina ya KIA, kila mwana Simba aliamini tunachukua ubingwa baada ya kutoka sare ugenini, mechi ya marudiano Dar es Salaam walifungwa 2-0.
“Mechi ilikuwa na tension, hata muda wa kuanza ulikuwa mgumu kwetu, tulicheza saa tisa alasiri jua kali kila mchezaji wa Simba alionekana amechoka kabla hata ya mechi, lakini ni kwa sababu ya kusumbuliwa, tulikuwa hatulali kambini, viongozi walitusumbua sana,” anasema.
Baada ya kufungwa kila mchezaji aliambulia gari aina ya Corola kutoka kwa mdhamini wao wakati ule.
Hivi sasa ni dereva wa basi la shule (School bus), huyu ni Malota Soma, mshambuliaji nyota wa zamani wa kikosi cha Taifa Stars na Simba.
Malota amejiajiri, anaendesha gari yake ambayo anaikodisha katika moja ya shule iliyopo Upanga kwa ajili ya kubeba wanafunzi, kazi ambayo anaifanya baada ya kustaafu soka mwaka 1998.
Malota anasema katika maisha yake ya miaka 10 kwenye soka, hawezi kudharau mchezo huo kwani umempa mwanga katika maisha.
“Pamoja na kwamba hatukuwa tukilipwa vizuri kama sasa, lakini soka nitaendelea kuiheshimu imenipa nyumba mbili Dar es Salaam na Morogoro na gari,” anasema.
Malota anasema yote hayo amefanya akiwa mchezaji wa Simba iliyomsajili akitokea Tumbaku mwaka 1980.
Bila Mogella asingecheza Simba
Tofauti na sasa, Malota anasema miaka ya nyuma wachezaji walikuwa wakipendekeza mchezaji gani asajiliwe na hata usajili wake Simba ulikuwa hivyo.
Anasema wakati anasajiliwa Simba alikuwa na miaka 19, walikwenda Norway kwenye mashindano akiwa na kikosi cha timu ya vijana ya Taifa chini ya kocha Mohammed Msumari.
“Tuliporejea, Mogella (Zamoyoni) alichukuliwa moja kwa moja na Simba, alipotua huko tu, alipendekeza na mimi nisajiliwe kwani tulikuwa wote timu ya Tumbaku.
Fenicha zampeleka Simba
Malota anasema viongozi wa Simba walimfuata na kufanya naye mazungumzo, alipangiwa nyumba na kuwekewa fenicha ili kukamilisha usajili wake na mwaka 1980 akatua rasmi Simba wakati huo mastaa wa Simba walikuwa Mussa Kihwelu, Abbas Kuka, Ezekiel Greyson ‘Juju Man’ na Nico Njohole.
“Sikuwa na hofu sababu nilijiamini tangu tukiwa shule ya msingi Kikundi ya Morogoro, nilikuwa na kombinesheni nzuri na Mogella kabla ya kwenda Reli na baadaye Tumbaku.
Anasema mtu aliyemfanya apende soka ni Omari Husein ambaye enzi wanacheza timu ya mtaani ya Jogoo ambayo ni miongoni mwa timu kubwa Morogoro nyingine ni Nyota, Mseto na Shujaa, Husein alikuwa mchezaji wa Taifa Stars.
“Wakati ule kuitwa Taifa Stars halikuwa jambo jepesi, hivyo alipokuwa akirudi Morogoro alikuwa chachu kwa wachezaji wengi nikiwamo mimi, kila mmoja alitamani kufikia levo yake,” anasema.
Anasema hata alipotua Simba hakuwa na mawazo ya kupata pesa yeye alitaka kucheza tu, hivyo walipompangishia nyumba na kumuwekea fenicha kwake ilikuwa ni usajili tosha.
Malota anasema miaka ya nyuma klabu ya Simba ilikuwa na matukio mengi, msimu haukupita bila tukio la kimgogoro kwa viongozi likiwamo la mwaka 1987 ambapo wachezaji walitakiwa wachague kati ya wazee na uongozi chini ya David Ngonya.
“Nakumbuka tulikuwa tunajiandaa na mashidano ya kombe la Nyerere, Dodoma wazee waliitaka timu na Ngonya ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Simba pia aliitaka.
“Siku moja kabla ya safari ya Dodoma tukiwa mazoezini zikaletwa tiketi za basi ambazo zilitoka kwa Ngonya na treni zilitoka kwa wazee.
“Tuliambiwa wanaotaka upande wa wazee waende katika tiketi za treni na wale wanaochagua upande wa uongozi waende upande wa tiketi za basi.
Anasema ulikuwa mtihani kwa wachezaji kwani ni kama waliwekwa mtegoni tena wakiwa mazoezini ikawalazimu wote kuchagua upande wa wazee walioongozwa na Sakwale.
“Tulikuwa mabingwa wakati wa kukabidhiwa zawadi pia zikaibuka vurugu wazee walitaka wakabidhiwe wao fedha na Ngonya pia akidai ndiye kiongozi ikabidi wachezaji tuingilie tukasema zawadi tunachukua wenyewe hakuna cha wazee wala uongozi, kweli tukapewa.
Anasema haikuishia hapo, mgogoro huo uliwahi kupelekea wachezaji kutoroshwa kambini siku moja kabla ya mechi na Yanga.
“Klabu ilikuwa na makomandoo wanaousapoti uongozi mwenyekiti akiwa Majid Seif na wengine walikuwa upande wa wazee.
“Tulikuwa kambini Sinza ambayo tuliwekwa na uongozi ikasukwa mipango na wazee baadhi ya wachezaji watoroshwe wapelekwe kwenye kambi nyingine ili tu wasicheze mechi na Yanga.
Anasema katika mpango huo makomandoo wa wazee waliwatorosha baadhi ya wachezaji, hivyo asubuhi walipoamka katika harakati za maandalizi ya kwenda uwanjani wakajikuta wako pungufu.
“Siku ya mechi hatukuwa na kipa tukasema basi ajitolee mmoja wetu awe kipa tucheze hivyo hivyo, ghafla saa nane mchana tukiwa klabuni tunajiandaa kwenda uwanjani akaibuka kipa wetu Omari Salehe Ombopa ambaye naye alitoroshwa akijitetea kuwa hakurubuniwa, lakini ile mechi nakumbuka haikuisha salama.
Simba waikwepa Yanga
Kila mchuma janga hula na wakwao, Malota anasema licha ya sekeseke hilo la ndani ya klabu kumalizika na timu kwenda uwanjani, lakini mechi ile haikuisha baada ya kuibuka vurugu, Simba wakigomea penalti waliyopewa Yanga.
Anasema katika mchezo huo, mshambuliaji wa Yanga, Abeid Mziba alipiga kichwa kwenye eneo la hatari na sentahafu wa Simba Twalib Hilal akautoa ule mpira kwa mkono.
“Iliku vurumai sisi tunasema ni faulo refarii aliitwa Bendera anasema ni penalti mechi haikuisha tuligoma tukatoka uwanjani, refarii akamaliza mechi tukiwa hatujafungana.
“Usiku katika vyombo vya habari, Said El Maamry akatangaza Yanga imepata pointi tatu na mabao mawili,” anasema.
Ukuta wa chuma
Licha ya uwezo mkubwa wa Malota katika kuzifumani nyavu, lakini anasema katika mechi ambayo alikuwa akikabwa na Adolph Rishard wa Pan African, Athumani Chama ‘Jogoo’ wa Yanga au Isihaka Hassan ‘Chukwu’ ilikuwa shughuli pevu.
“Hawa mabeki walikuwa wakitumia akili nyingi na nguvu kidogo katika ukabaji, tofauti na wengine mfano Kabunda na Aswile walikuwa Yanga, hawa jamaa walikuwa wakitumia nguvu sana wao kumtoa mtu damu ilikuwa kawaida, Aswile amewahi kunipasua usoni,” anasema nguli huyo.