Makocha akademi kupimwa
Muktasari:
- Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema usajili huo utasaidia Serikali kufahamu taarifa za makocha, taaluma zao na mwenendo wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema inataka makocha wote wanaofundisha katika akademi za soka visiwani hapa wasajiliwe rasmi ili kurahisisha utambuzi wao na kuimarisha usalama wa watoto wanaopata mafunzo katika vituo hivyo.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema usajili huo utasaidia Serikali kufahamu taarifa za makocha, taaluma zao na mwenendo wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Amesema si jambo jema watoto kufundishwa na watu ambao hawana taaluma inayotambulika wala taarifa zao hazifahamiki, kwani hali hiyo inaweza kuibua hofu kwa wazazi na walezi kuhusu usalama wa watoto wao.
"Tunataka kuona makocha wanaofundisha watoto wetu wamesajiliwa, wanastahiki na taarifa zao zinatambulika ili kulinda usalama wa watoto wakati wote wanapokuwa vituoni," amesema.
Dk Saada amefafanua uwezo wa mtoto kucheza mpira haumaanishi anaweza kujisimamia na kujilinda dhidi ya vitendo visivyofaa, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha haki na usalama wao vinalindwa.
Aidha, aliwasihi wazazi na walezi kuimarisha mawasiliano na watoto wao kwa kuzungumza nao mara kwa mara kuhusu vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kuwahamasisha kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo hivyo.
Amesema kuna baadhi ya watoto na vijana wanaofanyiwa vitendo visivyofaa katika akademi kwa kurubuniwa, hivyo Serikali haitaki hali hiyo iendelee kutokea Zanzibar.
Ameongeza usajili wa makocha utarahisisha ufuatiliaji wa mwenendo wao na kuwezesha mamlaka husika kuwafikia kwa haraka endapo kutatokea tatizo lolote katika akademi.