Kocha Gamera aizima KVZ
Muktasari:
- Bao pekee la Daddy Francis dakika ya 53, liliipa Chipukizi ushindi huo muhimu na kuifanya KVZ kutoka uwanjani vichwa chini.
BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ imeanza safari yake ya kisiwani Pemba kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Chipukizi inayofundishwa Suleiman Mohammed 'Gamera', kwenye Uwanja wa Gombani.
Bao pekee la Daddy Francis dakika ya 53, liliipa Chipukizi ushindi huo muhimu na kuifanya KVZ kutoka uwanjani vichwa chini.
Ushindi huo umeendeleza rekodi nzuri ya Kocha Gamera dhidi ya KVZ, ambaye amesema walitambua ubora wa wapinzani wao na kuamua kuingia kwa tahadhari, huku wakitumia mbinu za kuzuia mashambulizi na kuongeza kasi walipopata mpira.
"Tunapaswa kuongeza umakini kwani mechi ijayo, ni ngumu zaidi kuliko hii ya KVZ, hivyo bado nahitaji kushinda mechi ili kujiweka salama," amesema.
Amesema walitambua KVZ ni timu inayoweza kupata nafasi ya kutawala mechi, hivyo waliamua kuwadhibiti kipindi cha kwanza na kutumia nafasi zilizopatikana kuongeza kasi kipindi cha pili.
Amesema wachezaji wa KVZ walipoondoka katika maeneo yao ya ulinzi na kusogea mbele kutafuta bao la kusawazisha, Chipukizi ilipata nafasi ya kufanya shambulizi la haraka lililozaa bao la ushindi.
Ushindi huo unaifanya Gamera kuifunga KVZ mara mbili mfululizo katika mzunguko ya kwanza akiwa na timu tofauti.
Msimu uliopita wa 2025-2026 aliifunga akiwa na Fufuni kwa bao 1-0 katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Mao B, Unguja.
Kwa upande wake, kiungo mshambuliaji wa Chipukizi, Daddy ameendelea kuonyesha makali yake baada ya kufikisha mabao matatu na asisti tatu msimu huu.
Katika mechi nyingine, Uhamiaji iliichapa Mlandege mabao 3-0, Polisi ilitoka sare ya mabao 2-2 na Wembe, huku kinara wa ligi hiyo, Zimamoto, ikipoteza kwa kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Kipanga.