Mangungu nje uchaguzi Simba
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kutangaza majina ya waliokidhi vigezo vya awali, huku ikibainika kati ya wanachama 48 waliochukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo, wanane hawakujumuishwa kwenye orodha hiyo.
MWENYEKITI anayemaliza muda wake Simba SC, Murtaza Ally Mangungu ameondolewa kuendelea na mchakato wa kuwania nafasi hiyo baada ya jina lake kutokuwamo kwenye orodha ya awali ya wagombea 40 waliopita mchujo wa fomu uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo kutangaza majina ya waliokidhi vigezo vya awali, huku ikibainika kati ya wanachama 48 waliochukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa klabu hiyo, wanane hawakujumuishwa kwenye orodha hiyo.
Mangungu, ambaye alikuwa miongoni mwa watu saba waliojitokeza kuwania nafasi ya mwenyekiti, amekosekana katika orodha ya majina manne yaliyotangazwa na TFF, hatua inayofunga safari yake ya kutetea nafasi hiyo katika hatua hii ya mchakato.
Kwa mujibu wa orodha iliyotolewa leo Novemba 27, 2026, wagombea waliopitishwa awali kuwania nafasi ya Mwenyekiti ni Anindum Jonas Semu, Geoffrey Irick Nyange, Dk Seif Ramadhani Muba na Swedy Khamis Mkwabi.
Mbali na Mangungu, wengine wawili waliokuwa wamechukua na kurejesha fomu za nafasi hiyo lakini hawapo kwenye orodha mpya ni Mohamed Khamis Soloka na Selemani Haroub Said.
Kwa upande wa nafasi za wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, wagombea watano pia hawakujumuishwa kwenye orodha ya awali ya 36 waliotangazwa.
Waliokosekana ni Andrew Julius Tupa, Jamhuri Mussa Khwello ‘Julio’, Mariam Mussa Shemzigwa, Omari Juma Mazola na Pendo Aidan Mapugio.
Waliopitishwa ni Aaron Henry Mrina, Abdallah Rashid Mgomba, Alfred Martin Elia, Arnold Nzuatemi Nzali, Aziza Hussein Kaku, Christopher Kabalika Mwansasu na Damian Samweli Manembe.
Wengine ni Eli Achahofu Paulo, Enock Bwigane Mwasubila, Fadhili Mohamed Famonga, Farid Awadh Tamim, Francis Kumba Ndulane, Hamisi Omari Tika, Hassan Bakari Kakayoo, Hussein Ally Simba, Isabella Samwel Faya, Issa Masoud, Jonathan Wilisaan Nkya, Juma Abbas Pinto, Laurian Salvatory Mganga, Mariam Abdallah Ibrahim, Muhamadi Mohamed Hamisi, Rachel Juma Chagonja, Raphael Masunga Chegeni, Richard Shukia, Rodney Makamba Chiduo, Said Hassan Tully, Saidi Abdallah Njechele, Saleh Mohamed Afif, Salum Issaka Hamidu, Salum Kassim Maftah, Shukuru Athumani Mtego, Dk. Suleiman Serera, Ussi Salum Pondeza, Wilfred Elias Nyamwija na Yusuph Omary Yenga.
Mchujo huo umefanyika kwa kuzingatia Ibara ya 27(2) ya Katiba ya Simba, inayohusu ukaguzi wa fomu zilizorejeshwa na uhakiki wa sifa za wagombea ili kubaini kama wametimiza masharti ya kuwania nafasi walizoomba.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Uchaguzi, baada ya kutangazwa kwa orodha hiyo ya awali, mapingamizi dhidi ya wagombea yataanza kupokelewa kesho Jumamosi Novemba 28, 2026 na Jumapili Novemba 29, 2026, hatua itakayotoa nafasi kwa wahusika kuwasilisha hoja zao kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi. Uchaguzi Mkuu wa Simba SC umepangwa kufanyika Januari 30, 2027, huku mchakato ukiendelea kupitia hatua mbalimbali kabla ya kupatikana kwa orodha ya mwisho ya watakaoshiriki kuwania nafasi za uongozi wa klabu hiyo.