Makaga, Ngai waamsha shangwe uchaguzi Yanga
Muktasari:
- Makaga na Ngai walipokelewa kwa shangwe na nderemo kila mmoja aliposimama kuzungumza mbele ya wanachama, hali iliyosababisha shughuli za mkutano kusimama kwa zaidi ya dakika moja kutokana na kelele za kushangilia.
Wagombea wa nafasi za Kamati ya Utendaji ya Yanga, Yanga Makaga na Alex Ngai, wameibua shamrashamra kubwa kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo walipopewa nafasi ya kuomba kura katika Mkutano Mkuu unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Makaga na Ngai walipokelewa kwa shangwe na nderemo kila mmoja aliposimama kuzungumza mbele ya wanachama, hali iliyosababisha shughuli za mkutano kusimama kwa zaidi ya dakika moja kutokana na kelele za kushangilia.
Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Yanga, Malangwe Mchungahela, alilazimika kuwaomba wanachama watulie ili kuwapa wagombea hao nafasi ya kuwasilisha salamu zao na kuomba kura.
Makaga na Ngai ni miongoni mwa wagombea 15 wanaowania nafasi katika Kamati ya Utendaji ya Yanga, huku wakitetea nafasi zao pamoja na Seif Gulamali, Munir Said Seleman na Rodgers Gumbo.
Wagombea wengine wanaowania nafasi hizo ni Injinia Mustapha Himba, Prisca Kishamba, Julius Koyi, Saady Khimji, Freddy Mahembe, Mshindo Hamza Msola, Issa Mangungu, Farid Afif, Mohammed Mwenda na Mzee Mwinyi.
Wagombea hao walifanya kampeni kwa kipindi cha siku nane, kuanzia Julai 25 hadi Agosti 1, 2026, wakitumia majukwaa mbalimbali kueleza sera zao na kuwashawishi wanachama kuwapa ridhaa ya kuwatumikia.
Kwa mujibu wa Katiba ya Yanga, wagombea watano pekee ndio watachaguliwa na wanachama kuunda Kamati ya Utendaji, huku wajumbe wengine wawili wakiteuliwa na Rais wa klabu.