Magori, Mangungu wazika tofauti Simba, waelekeza nguvu msimu mpya
Muktasari:
- Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo, Agosti 4, viongozi hao wamethibitisha kusimamisha kwa muda matukio na maazimio yote yaliyohusu Baraza la Wadhamini wa klabu, wakisema suala hilo litashughulikiwa baadaye ili kutoa nafasi kwa mambo ya msingi yanayoikabili Simba kwa sasa.
Viongozi wakuu wa Simba, Crescentius Magori na Murtaza Mangungu, wameamua kuweka kando tofauti zao na kuahidi kushirikiana kwa maslahi ya klabu, kufuatia kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kilichofanyika jana, Agosti 3, 2026.
Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa leo, Agosti 4, viongozi hao wamethibitisha kusimamisha kwa muda matukio na maazimio yote yaliyohusu Baraza la Wadhamini wa klabu, wakisema suala hilo litashughulikiwa baadaye ili kutoa nafasi kwa mambo ya msingi yanayoikabili Simba kwa sasa.
Hatua hiyo inalenga kurejesha utulivu ndani ya klabu wakati huu ambao Simba inaendelea na maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bodi ya Wakurugenzi sasa itaelekeza nguvu zake katika kukamilisha usajili wa wachezaji, maandalizi ya Simba Day, mchezo wa Ngao ya Jamii, pamoja na kampeni ya Ligi Kuu ya NBC na mashindano mengine ya msimu wa 2026/27.
Magori ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi, na Makamu wake Mangungu wamewataka wanachama, mashabiki na wadau wa Simba kuweka pembeni tofauti zozote na kuendelea kuiunga mkono klabu hiyo, wakisisitiza kuwa mshikamano ndiyo msingi wa kufikia malengo makubwa waliyojiwekea msimu huu.
Taarifa hiyo ya pamoja inaashiria hatua ya maridhiano ndani ya uongozi wa Simba, huku macho ya wanachama yakielekezwa kuona namna umoja huo utakavyoisaidia klabu kufanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.