Mabondia wa Tanzania wanavyopigwa makusudi Ulaya-1

Bondia wa uzito wa kati Thomas Mashali
Muktasari:
Mwili wake wa wastani unazungumza kwamba huyu ni mwanamazoezi ambaye usoni anaonekana kuwa na makovu hafifu, lakini hafichi tabasamu la kila wakati.
NAKUTANA na kijana wa makamo pale Magomeni Kagera jijini Dar es Salaam. Uso wake unaonekana una bashasha huku akizirudisha nyuma rasta zake zilizotokeza nje ya kofia nyeusi aliyovaa.
Mwili wake wa wastani unazungumza kwamba huyu ni mwanamazoezi ambaye usoni anaonekana kuwa na makovu hafifu, lakini hafichi tabasamu la kila wakati.
Baada ya kutafutana kwa muda mrefu, hatimaye nakutana nawe, huyi si mwingine bali ni bondia wa uzito wa kati Thomas Mashali (33) ambaye ananiomba niueleze umma kwamba jina lake ni Thomas Fabian Mashale isipokuwa wakati anaanza ngumi vyombo vya habari vilikosea kuandika jina lake la mwisho.
Machoni anaonekana ni mdadisi wa mambo, baada ya kunikaribisha ananiomba afanye mazoezi kisha tuzungumze mambo muhimu kuhusu ngumi ambayo anadhani mdomo wake unaweza kubadili mchezo huo endapo atayaweka wazi.
Baada ya mazoezi ya dakika 90, kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 12:30, Mashale ananikaribisha katika kiti maalumu kinachoonekana kama cha wageni katika sehemu ya mazoezi ‘gym’ iliyopo ghorofa ya sita katika jengo moja Magomeni Kagera.
“Hapa ndipo mahala ninapofanyia mazoezi yangu na ukisikia nimepoteza pambano au kushinda ujue hapa panahusika,” anasema Mashali huku akijiweka vizuri katika chuma kimoja ambacho ni maalumu kwa mazoezi.
Kabla hatujaanza mazungumzo, Mashali anamtuma maji ya kunywa kijana mmoja ambaye analazimika kushuka hadi chini ya jengo hilo kisha anarejea na mazungumzo yanaanza.
Lengo kuu la kukutana na Mashali ni kutaka kujua kwa undani jinsi mabondia wa Tanzania wanavyotumika kupandisha viwango mabondia wa nchi za Ulaya huku wakilipwa ujira mdogo.
Lakini kabla ya mazungumzo hayo, Mashali anaanza kwa kunieleza kwamba licha ya kuanza ngumi mwaka 1999 baada ya kuvutiwa na mdogo wake aitwaye Charles Mashali aliyekuwa bondia, pia anasema kitendo cha kufungwa jela mwaka 2008 kilichangia kumwongezea hamasa ya kupigana ulingoni.
Juni 2008, Mashali alihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kumpiga mtu akiwa katika baa moja Manzese baada ya kuchokozwa.
“Bondia haruhusiwi kumpiga mtu ambaye hana mazoezi katika maisha ya kawaida, kwani haifai kupigana na mtu ambaye unajua hana mazoezi kwa sababu utakuwa unamwonea tu.
“Lakini siku hiyo nilikuwa nimepata bia mbili tatu hivi na nikashindwa kuzuia hasira zangu pindi kijana mmoja aliponichokoza bila kujua nina uwezo gani wa kupigana. Nilimpiga ngumi akavunjika taya, nilikaa ndani hadi mahakama iliponihukumu,” anasema Mashali.
Maisha ya jela
“Jela kuna ubabe na wale wababe wote wa huko ni lazima wajue ngumi. Sasa kuingia kwangu Keko hakukunipa shida, kwani wahuni wengi walinijua mimi nani na nafanya nini. Niliishi nao vizuri, lakini kuna wakati ilibidi niwe nawasaidia wanyonge nilioona wanaonewa bila sababu,” anasema.
“Sikuwahi kumpiga mtu jela japokuwa nimewahi kutoa vitisho kwa watu waliokuwa hawawatendei vizuri wenzao. Nilijifunza vitu vingi kupitia maisha ya jela na ndiyo maana hadi sasa mimi ni raia mtiifu na siwezi tena kumpiga mtu mitaani.”
Mabondia wa Tanzania
Mashali anaeleza kuwa mabondia wengi wa Tanzania hawajaenda shule, hivyo hawana ufahamu wa mambo mengi ya msingi yanayowahusu hasa mikataba ya kupigana, mbaya zaidi ile inayoandikwa kwa Lugha ya Kiingereza.
“Ukweli mabondia wengi hawana elimu na ndiyo maana unawaona wanafanya kazi ambazo si rasmi, wengine wanapiga debe wengine wakiamka asubuhi hadi jioni hakuna wanalofanya wakitegemea ngumi tu,” anaweka wazi.
“Kutojua lolote ndiko kunakofanya mabondia kupigana kwa ujira mdogo na wakati mwingine mapromota kuwadhulumu haki zao na hawajui hata mahala pa kwenda kulalamika. Tazama hivi bondia kama ***** (analitaja jina la bondia maarufu) ni mtu wa kudhulumiwa eti kisa tarehe ya kusaini mkataba ilikosewa? Hadi leo hajalipwa wanaisubiri hiyo tarehe iliyokosewa makusudi.
Kuelekea pambano la bondia wa Tanzania, kunatakiwa maandalizi ya wiki tatu kujenga mwili tu kwa kufanya mazoezi magumu ikiwemo kupanda milima, ngazi na kukimbia mchangani halafu wiki mbili nyingine hufanya mazoezi ya mbinu za ufundi wa kupigana kulingana na mpinzani wako.
Upangaji wa matokeo Ulaya
Yawezekana upangaji matokeo umekuwa maarufu katika soka, lakini hata katika ngumi wapo mabondia wanaopanga matokeo hasa wa Ulaya na Amerika wanapoelekea kupambana katika pambano kubwa.
Mashali anasema kuna mabondia wengi wa Kitanzania wanaopanga dili ili kwenda kupigwa Ulaya na kupandisha viwango vya mabondia wa mataifa mengine.
Unataka kujua kinachoendelea kuhusu upangaji wa matokeo wa mabondia wa Tanzania huko Ulaya? Ungana na mwandishi wetu katika mfululizo wa makala haya yatakayoendelea Alhamisi Ijayo.