Maafande wamvutia waya Kipenye
Muktasari:
- Kiungo huyo amefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba wake na kikosi Cha Namungo baada ya kukitumikia kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne, tangu ajiunge nacho Julai 8, 2025 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship.
MABOSI wa maafande wa JKT Tanzania, wameanza mazungumzo ya kupata huduma ya aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Namungo FC, Cyprian Kipenye wakati dirisha dogo la Januari 2027, litakapofunguliwa baada ya nyota huyo kwa sasa kutokuwa na timu.
Kiungo huyo amefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba wake na kikosi Cha Namungo baada ya kukitumikia kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne, tangu ajiunge nacho Julai 8, 2025 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship.
Mtu wa karibu na mchezaji huyo, ameliambia Mwanaspoti klabu mbalimbali zimeonyesha nia ya kumuhitaji Kipenye katika dirisha dogo la Januari 2027, ingawa, hadi sasa JKT Tanzania ndio iko mstari wa mbele japo hakuna muafaka rasmi.
“Ni kweli JKT Tanzania imeonyesha nia ya kumuhitaji lakini hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande zote mbili kwa maana ya klabu na kambi ya mchezaji, nadhani kwa sasa tuwe na subira kwa sababu muda bado upo,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kipenye amesema baada ya kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake na Namungo, kwa sasa ni mapema kuweka wazi timu atakayoichezea, ingawa kuna mazungumzo yanaendelea na baadhi ya timu zilizoonyesha nia ya kumuhitaji.
Kipenye aliyecheza timu mbalimbali za Ihefu FC kwa sasa Singida Black Stars, Dodoma Jiji, Biashara United, Songea United na Namungo FC, msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu 2025-2026, alichangia mabao matano akifunga matatu na asisti mbili.