Kipenye atimka Namungo FC
Muktasari:
- Nyota huyo alijiunga na Namungo FC, Julai 8, 2025, kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, ingawa, amefikia uamuzi wa kusitisha kandarasi yake iliyokuwa inafikia mwishoni mwa msimu wa 2026-2027.
KIUNGO mshambuliaji wa Namungo FC, Cyprian Kipenye amefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba wake na kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, baada ya kukitumikia kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi minne tangu ajiunge nayo.
Nyota huyo alijiunga na Namungo FC, Julai 8, 2025, kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, ingawa, amefikia uamuzi wa kusitisha kandarasi yake iliyokuwa inafikia mwishoni mwa msimu wa 2026-2027.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kipenye alisema amefikia uamuzi huo kwa maslahi yake binafsi kwa ajili ya kuangalia sehemu nyingine ya kupata changamoto mpya, huku akiushukuru uongozi, benchi la ufundi na wachezaji wenzake kwa ushirikiano wao.
“Ni uamuzi mgumu kwangu kuuchukua ila wenye nia nzuri, nawashukuru viongozi kwa imani kubwa waliyonipa tangu mara yangu ya kwanza najiunga nao hadi ninapositisha mkataba wangu, watabakia katika kumbukumbu zangu maishani,” alisema Kipenye.
Nyota huyo alianza safari yake ya soka katika kikosi cha vijana cha Simba B, chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nico Kiondo, ikiwa ni siku chache tu tangu amalize masomo yake ya kidato cha nne kipindi hicho akitoka kwenye Mkoa wa Katavi.
Kipenye aliyecheza timu mbalimbali za Ihefu FC kwa sasa Singida Black Stars, Dodoma Jiji, Biashara United, Songea United na baadaye kujiunga na Namungo FC, msimu wake wa kwanza wa Ligi Kuu 2025-2026, alichangia mabao matano ya kikosi hicho.
Katika msimu huo wa 2025-2026, Kipenye alifunga mabao matatu na kuasisti mawili, akichangia matano kati ya 25, ya kikosi hicho kizima, ambacho kilimaliza nafasi ya 10 na pointi 34, baada ya kushinda mechi zake saba, sare 13 na kupoteza 10.
Tangu kuanza kwa msimu wa 2026-2027, nyota huyo ameshindwa kuendeleza kiwango kizuri kutokana na kuandamwa na majeraha ya mara kwa mara, jambo lililochangia kukaa nje kwa sasa na kufikia uamuzi wa kusitisha mkataba wake uliobaki kikosini.