Maabad awekewa mtego Mashujaa
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Coastal Union Julai 11, 2022, akitokea KVZ FC ya visiwani, Zanzibar, mkataba wake na timu hiyo ya jijini, Tanga unafikia tamati rasmi Januari 2027, jambo ambalo limewafanya mabosi wa Mashujaa FC kuanza kumfuatilia.
MSHAMBULIAJI nyota wa kikosi cha Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Maabad Maulid, yuko katika hatua za mwisho za kujiunga na maafande wa Mashujaa FC ya mjini Kigoma, wakati dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa rasmi kuanzia Januari 2027.
Nyota huyo aliyejiunga na Coastal Union Julai 11, 2022, akitokea KVZ FC ya visiwani, Zanzibar, mkataba wake na timu hiyo ya jijini, Tanga unafikia tamati rasmi Januari 2027, jambo ambalo limewafanya mabosi wa Mashujaa FC kuanza kumfuatilia.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Mashujaa FC, zimeliambia Mwanaspoti, Maabad ni miongoni mwa washambuliaji wanaopigiwa hesabu katika dirisha dogo la Januari 2027, ambapo mazungumzo ya awali yameanza na yamefikia katika hatua nzuri zaidi.
“Ni kweli Maabad tunazungumza naye na tutakapofikia makubaliano rasmi tutaweka wazi, ni miongoni mwa washambuliaji bora wazawa katika nchi yetu na ni pendekezo la benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Amani Josiah,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maabad alisema kwa sasa malengo yake ni kuendelea kufanya vizuri na timu hiyo katika mechi za Ligi Kuu Bara na mashindano mengine, japo ikiwa kutakuwa na taarifa zozote zinazomhusu ataweka wazi kwa mashabiki zake.
“Mawazo yangu kwa sasa yapo hapa Coastal, hapa ndiyo kituo changu cha kazi kama kutakuwa na ishu nyingine baadaye nitaweka wazi.’’
Licha ya kauli ya mshambuliaji huyo, ila Mwanaspoti linatambua mazungumzo kati ya pande mbili kwa maana ya mchezaji na Mashujaa FC yanaendelea vizuri, huku mambo machache yakiwa yamebakia kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote za usajili.
Maabad alijiunga na Coastal Union, Julai 11, 2022, akitokea KVZ FC ya Zanzibar ambapo alikuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo, akianza na msimu wa 2020-2021, alipofunga mabao 17, kisha na msimu uliofuata wa 2021-2022, akafunga mabao 21.
Tangu nyota huyo ajiunge na Coastal Union, msimu wake bora katika Ligi Kuu Bara ni uliopita wa 2025-2026, ambao alifunga mabao 10, huku msimu huu wa 2026-2027, tayari ameifungia matatu, akionyesha kiwango kizuri cha kuvutia kwa kikosi hicho.