Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kimoto achekelea kichapo kwa Azam

Muktasari:

  • Ushindi huo wa mabao 4-2 umevunja mfululizo wa matokeo mabaya ambao Singida ilikuwa imeupata, ikiwamo kupoteza kwa mabao 0-1 dhidi ya Mbeya City, Novemba 3, 2026.

KOCHA wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana hadi dakika za mwisho na kuibuka na ushindi dhidi ya Azam FC, akisema matokeo hayo yamekuwa faraja kubwa kwa kikosi chake baada ya kupitia kipindi cha matokeo yasiyoridhisha.

Ushindi huo wa mabao 4-2 umevunja mfululizo wa matokeo mabaya ambao Singida ilikuwa imeupata, ikiwamo kupoteza kwa mabao 0-1 dhidi ya Mbeya City, Novemba 3, 2026.

Kabla ya mchezo huo dhidi ya Azam, Singida ilikuwa imecheza mechi 10 za ligi, ikishinda nne, sare mbili na kupoteza nne, ikiwa na pointi 14 na kukaa nafasi ya tisa. Ushindi wa Chamazi umeifikisha pointi 17 baada ya mechi 11.

Katika mchezo huo, Azam ilianza kwa kasi na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-1, kupitia Feisal Salum na Zidane Sereri. Hata hivyo, Singida ilirejea kipindi cha pili kwa nguvu, Mwashinga akisawazisha dakika ya 52 kabla ya Jonathan Sowah kufunga mabao mawili dakika ya 68 na 73.

Kocha huyo alizungumza na Mwanaspoti alisema kuwa, pamoja na kukosolewa kutokana na mwenendo wa timu, hakubaliani na mtazamo kwamba kikosi chake kimekuwa kikicheza vibaya kila kinapopoteza mchezo.

Akizungumzia kipigo cha mchezo uliopita dhidi ya Mbeya City, Kimoto alisema matokeo hayakuakisi kikamilifu kiwango ambacho wachezaji wake walionyesha uwanjani.

“Ninawapongeza sana wachezaji wangu kwa sababu hawakukata tamaa. Tulikuwa nyuma, lakini waliendelea kupambana na kutafuta ushindi. Hicho ndicho nilichokuwa nakihitaji kutoka kwao,” alisema Kimoto.

Aliongeza kuwa, “Watu wamekuwa wakitusema vibaya kutokana na matokeo, lakini hata kwenye mchezo tuliopoteza dhidi ya Mbeya City tulicheza vizuri. Si kila tunapopoteza maana yake timu haijacheza vizuri.”

Kimoto alisema kabla ya mchezo dhidi ya Azam, benchi la ufundi na wachezaji walikubaliana kuweka nguvu zao katika kutafuta matokeo bila kuruhusu changamoto zinazowazunguka kuwavuruga.

“Kabla ya mchezo tulikaa na kukubaliana jambo moja, kwamba tunapaswa kupigana. Tulijua kuna changamoto ambazo tunaweza kukutana nazo, lakini tulikubaliana tusizipe nafasi ya kutuzuia kupata matokeo mazuri,” alisema.

“Ushindi huu umetupa nguvu kubwa sana. Unaposhinda mchezo mgumu namna hii, wachezaji wanapata imani zaidi. Tunaenda kwenye mchezo mwingine tukiwa na morali nzuri na tunajua tunahitaji kuendeleza hali hii.” alisema kocha huyo ambaye timu yake sasa inaweka nguvu kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Union Maniema.

Kimoto, ambaye anaifahamu vizuri Union Maniema kutokana na historia yake ya kufanya kazi na timu hiyo, amesema kikosi chake kinapaswa kutumia hali nzuri iliyotokana na ushindi huo kama msingi wa maandalizi ya mchezo unaofuata.

Mchezo dhidi ya Maniema Union una uzito wa kipekee kwa Kimoto kwa sababu aliwahi kuifundisha timu hiyo ya DR Congo na kuifikisha hatua ya robo fainali ya mashindano ya CAF msimu uliopita. Sasa anakutana nayo akiwa upande wa Singida, katika mchezo wa kwanza wa kundi C uliopangwa kufanyika kati ya Novemba 27 na 29, 2026.