Maabad asaka rekodi mpya Ligi Kuu
Muktasari:
- Coastal Union iliyoanza msimu kwa kusuasua ikicheza mechi nne mfululizo bila ya ushindi ikiambulia vichapo vitatu na sare moja, imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Polisi Tanzania iliposhinda 2-1 ugenini.
MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Maabad Maulid Maabad, amechekelea kuanza kufunga mabao katika Ligi Kuu Bara msimu huu, huku akibainisha kwamba anataka kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita.
Coastal Union iliyoanza msimu kwa kusuasua ikicheza mechi nne mfululizo bila ya ushindi ikiambulia vichapo vitatu na sare moja, imefanikiwa kupata ushindi wake wa kwanza dhidi ya Polisi Tanzania iliposhinda 2-1 ugenini.
Katika mchezo huo wa raundi ya tano uliochezwa Septemba 6, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Maabad ndiye aliibuka shujaa akifunga mabao yote akiwa ndiyo amefungua akaunti yake ya mabao msimu huu, huku msimu uliopita akitupia 10.
Akizungumza na Mwanaspoti, Maabad amesema matokeo hayo ni juhudi na ushirikiano wa pamoja kikosini, akieleza kuwa kwa sasa wanaendelea kujipanga na michezo iliyo mbele yao kuendeleza makali.
Alikiri kuwa, ligi si nyepesi na inahitaji kupambana bila kuchoka akichekelea ubora wake na kuipa matokeo mazuri timu hiyo, akiahidi makubwa zaidi kikosini akiwaomba sapoti mashabiki.
“Hatujaanza vizuri, lakini tunaamini baada ya kupata ushindi nguvu imerejea upya, hatujawahi kukata tamaa na matarajio yangu ni kuona timu inafanya vizuri kila mchezo, nashukuru kiwango kimeendelea kuwa kizuri kwangu,” amesema straika huyo.
Ameongeza kuwa, kwa sasa wanaendelea kusahihisha makosa yao lakini kuboresha maeneo yote kuhakikisha mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania wanaendeleza makali yao ili kujiweka nafasi nzuri. Kuhusu kasi ya ufungaji mabao, staa huyo kutoka Zanzibar, amesema baada ya kutupia, anahitaji kuvuka idadi ya msimu uliopita akieleza kuwa kila mchezo kwake ni kutumia vyema nafasi anazopata.
“Tunaamini kwa ushirikiano na kujituma kwetu tukifuata maelekezo ya kocha tutafanya vizuri na kufikia malengo, ligi si nyepesi na lazima tujitoe kuipambania timu kwanza,” amesema.
Straika huyo alijiunga na Coastal Union msimu wa 2022-2023 akitokea KVZ baada ya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar kwa mabao 19. Huu ukiwa ni msimu wa tano kucheza Ligi Kuu Bara, ana jumla ya mabao 24. Rekodi zinaonyesha msimu wa 2022-2023 alifunga mabao manne, 2023-2024 (mabao matatu), 2024-2025 (mabao matano), 2025-2026 (mabao 10) na msimu huu amefunga mabao mawili.