Lwandamina aifumua upya Azam FC
MASHABIKI wa Azam hawaielewi timu yao ikipata sare ya nne mfululizo na katika mechi sita za mwisho za Ligi Kuu Bara hawaujui ushindi wowote lakini kocha wao mpya George Lwandamina atafanya mabadiliko dirisha dogo.
Azam mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 5 walipoichapa Dodomo Jiji ka mabao 3-0 baada ya hapo wamekuwa wakipata matokeo ya kushtua huku sehemu kubwa ikiwa sare lakini pia wakipoteza mara mbili.
Kocha wao mpya Lwandamina ambaye ameiongoza timu hiyo katika mechi mbili akiambulia pointi mbili amefunguka kwamba anahitaji kuingiza watu wapya katika kikosi chake.
Akizungumza na Mwanaspoti Lwandamina alisema kuna sababu kubwa kwake kuingia sokoni katika dirisha dogo la usajili na kwanza anahitaji straika mabao atakayekuja kuziba nafasi ya Prince Dube ambaye bado yuko nje akiuguza mkono wake.
Lwandamina raia wa Zambia alisema hatua ya pili katika usajili huo pia atahitaji kiungo mmoja mkabaji atakayekuja kusaidiana na Mnyarwanda Ally Niyonzima.
“Tunahitaji mshambuliaji wa kati mwenye rekodi nzuri na uwezo wa kufunga,nimeona kazi aliyoifanya Dube ni mtu muhimu tunamkosa lakini hatuwezi kuendelea kuwaza kutokuwepo kwake tunahitaji mtu mwingine atakayekuja kuendelea kutufungia kusaidiana na wengine,”alisema kocha huyo za zamani wa Zesco na Yanga.
“Kwenye kiungo nafikiria kutafuta kiungo mwingine wa eneo la ukabaji tuna Niyonzima( Ally) lakini tunahitaji uzito zaidi eneo hilo.
Aidha Lwandamina alisema maboresho hayo pia yataendelea katika safu yake ya ulinzi kwa kuingiza mabeki pamoja na kipa mwenye makali zaidi.
“Tunafunga magoli lakini hatujaweza kulinda vizuri ushindi ambao tunataka kutengeneza, tunahitaji watu wapya katika mabeki lakini pia hata eneo la makipa nako tutaliangalia upya kuna changamoto.