Ligi ya Netiboli Zanzibar kuanza leo
Muktasari:
- Timu zitakazoshiriki nane ni za wanawake ambazo ni KVZ, Mafunzo, Zimamoto, Bandari, JKU, Afya, Chake Stars na Nungwi, huku mbili za wanaume ni The Talent na Chake Boys.
LIGI Kuu ya Netiboli Zanzibar, inatarajiwa kuanza leo Jumatatu katika Uwanja wa Gymkhana kisiwani Unguja huku timu 10 zikishiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa na ushindani na kuibua vipaji.
Timu zitakazoshiriki nane ni za wanawake ambazo ni KVZ, Mafunzo, Zimamoto, Bandari, JKU, Afya, Chake Stars na Nungwi, huku mbili za wanaume ni The Talent na Chake Boys.
Mchezo wa ufunguzi utazikutanisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo, KVZ dhidi ya Mafunzo, pambano hilo linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Katibu Msaidizi wa Chama cha Netiboli Zanzibar (Chaneza), Fredrick Apiuwe, amesema maandalizi yote ya ligi hiyo yameshakamilika na chama kipo tayari kusimamia vizuri.
Pia, Katibu huyo amesema chama hicho kimeshakamilisha maandalizi ya waamuzi, ratiba ya michezo na usimamizi wa mashindano hayo ili kuhakikisha ligi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria.
"Ligi hii inalenga kuendeleza mchezo wa Netiboli Zanzibar na kutoa fursa kwa wachezaji kuonesha vipaji vyao," amesema.