Pemba inavyonawiri na viwanja vya kisasa
Muktasari:
- Pemba ya jana siyo ya leo. Kwa ambao hawajawahi kufika kisiwa hicho chenye asili ya ukarimu, kilichozungukwa na Bahari ya Hindi na kujengeka kwa milima mikubwa na mabonde, ni wakati sahihi wa kufika.
UNAWEZA kusema kwamba zile dhana na imani za kuwa Pemba haiwezi kujengwa, hususan kwa upande wa michezo, kwa sasa mambo yamekuwa tofauti na matarajio ya kila mmoja. Kati ya kundi la watu 100, pengine unaweza kupata 10 tu ambao waliamini ipo siku kisiwa hiki kitakuwa na mabadiliko makubwa kwenye miundombinu ya michezo.
Pemba ya jana siyo ya leo. Kwa ambao hawajawahi kufika kisiwa hicho chenye asili ya ukarimu, kilichozungukwa na Bahari ya Hindi na kujengeka kwa milima mikubwa na mabonde, ni wakati sahihi wa kufika.
Mwanaspoti halikutaka kusimuliwa juu ya mabadiliko hayo, bali lilifunga safari kutoka Unguja hadi Pemba kushuhudia mageuzi katika sekta ya michezo. Naam! Zile neema zimefika kwa wakati sahihi. Kwa sasa kazi si ya Serikali tena, bali vijana wenye vipaji wavioneshe na kuvikuza maana miundombinu ya viwanja vya aina zote imewekwa.
Kwa kifupi Pemba haijamuacha mtu nyuma. Kuanzia viwanja vya mpira wa miguu, viwanja vya mpira wa kikapu, wavu, handiboli na voliboli, wote wamepewa nafasi. Katika miaka ya nyuma, viwanja vilivyokuwa vinatumika kwa mashindano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu ya Zanzibar havikuwa vinaridhisha wala kukidhi mahitaji ya wachezaji. Hivyo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikaamua kwa makusudi kuwekeza fedha dola za Marekani milioni 51 sawa na Sh127.7 bilioni kwa ujenzi wa viwanja vya michezo vya wilaya na mikoa.
Mradi huo unatekelezwa kwa viwanja 17 katika wilaya 11 na mikoa mitano ya Unguja na Pemba. Kati ya viwanja hivyo vinavyojengwa, 13 vimeshakamilika na vinne vinaendelea kujengwa, ambapo Pemba vipo sita; kati ya hivyo viwili ni vya mkoa na vinne vya wilaya.
GHARAMA VIWANJA VYA PEMBA
Kwa upande wa Pemba kuna viwanja vinne vya wilaya vinavyojengwa ambavyo vinagharimu Sh21.8 bilioni, huku viwanja vya mkoa daraja la pili vikigharimu Sh8.3 bilioni na vya mkoa daraja la kwanza Sh12 bilion, huku jumla ya fedha ikiwa ni ni Sh42 bilioni.
Mwanaspoti imefika kwenye Ofisi ya Ofisa Michezo Wilaya ya Chake Chake na Kaimu Wilaya ya Mkoani, Issa Adam Hamza, zilizopo Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba, ambaye ameeleza mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanja hivyo na muamko wa michezo kwa wananchi kisiwani hapa.
Ofisa huyo anasema kati ya viwanja hivyo vyenye hadhi tofauti, vile vya wilaya vinajulikana kama daraja la tatu. Kwa Wilaya ya Chake Chake kipo Gombani na Wilaya ya Mkoani kipo Ukutini, huku kiwanja cha Mkoa wa Kusini Pemba chenye hadhi ya daraja la pili (Type Two) kikiwa Kangani.
Pia, uwanja cha Wilaya ya Micheweni upo Micheweni na Wete upo Pandani, huku cha Mkoa wa Kaskazini Pemba ukiwa Kinyikani wenye hadhi ya daraja la kwanza (Type One). “Viwanja hivyo vina uwezo wa kuchukua mashabiki 500, lakini Type Two inakuwa na uwanja wa mpira wa miguu na kiwanja kimoja cha michezo ya mikono ikiwemo netiboli, mpira wa kikapu, voliboli na wavu, pamoja na njia nne za kukimbilia, taa na vyumba vya kubadilishia nguo, na huu ni uwanja wa Kangani,” anasema. Hivyo, Ofisa Issa anasema kwa sasa viti kwa ajili ya mashabiki havijajengwa katika awamu hiyo ya kwanza, lakini baada ya kukamilika wanatarajia kuanza ujenzi wa sehemu hizo.
Pia, Ofisa huyo anasema kwa upande wa Type One vigezo vinaongezeka kwa kuwa na viwanja viwili vya michezo ya mikono na kimoja cha mpira wa miguu, njia nane za kukimbilia na hosteli kwa timu zinazohitaji kulala hapo, na uwanja huo upo Kinyikani.
Anasema katika viwanja hivyo kuna chumba maalumu cha kubadilishia nguo kwa wachezaji chenye siti 23, vyoo vitano vya haja ndogo na kubwa na vyoo vitatu vya kusimama pamoja na sehemu ya kujisafishia baada ya kumaliza haja. Pia, anasema chumba hicho kina sehemu ya meneja, waamuzi na madaktari.
Ofisa huyo anasema kwa upande wa Pemba, viwanja viwili pekee ambavyo havijakamilika ni Ukutini na Kinyikani na vipo kwenye hatua za mwisho, na kwamba viwanja ambavyo vimekamilika vitakuwa chini ya mwendeshaji Bahari Leisure kwani tayari ameshakabidhiwa.
Lakini awali viwanja hivyo vilipokuwa chini ya usimamizi wao walikuwa wanavikodisha kwa gharama ya Sh100,000 kwa timu zilizokuwa zinahitaji kuvitumia kwa mechi, isipokuwa mazoezi walikuwa wanaruhusiwa bure.
Anasema fedha hiyo inatozwa kwa timu zote mbili kwa kuwa kila timu hutoa Sh50,000 na hivyo kufikia kiwango hicho. Amesema Uwanja wa Gombani ndio utakaokuwa chini ya wizara hiyo kuanzia usimamizi na utunzaji kwa sababu ndio uwanja mama kwa hapa Kisiwani Pemba.
HOFU, MWAMKO
Anasema baada ya kujengwa viwanja hivyo wanategemea vijana kuwa na muamko mzuri wa michezo, lakini wanahofu kwa sababu kutatokea mvutano baina ya wachezaji na mwendeshaji.
Anafafanua kuwa mvutano huo unaweza kutokea kwa timu kuhitaji kucheza kwenye viwanja vya kisasa huku zikikosa vigezo vya kutumia viwanja hivyo au kushindwa kumudu gharama zake.
Anasema anaamini kwamba si kila timu itapata nafasi ya kucheza katika viwanja hivyo, jambo ambalo linaweza kupunguza hamasa. Hivyo amemshauri mwendeshaji huyo kuweka gharama itakayokwenda sambamba na vipato vya wananchi ili waweze kuzimudu.
Anasema licha ya hayo yote bado hamasa ipo kwani kila mmoja anatamani kucheza kwenye viwanja vilivyojengwa.
USALAMA WA WAAMUZI
Ofisa huyo anasema viwanja vinavyojengwa vimezingatia vigezo vya kimataifa vinavyohitaji kuzungushwa uzio ili kutenganisha mashabiki, wachezaji na waamuzi na itasaidia kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa waamuzi kabla, wakati na baada ya mechi na kudhibiti matukio ya mashabiki kuwapiga waamuzi.
Baada ya kufanyika maboresho hayo, Wizara ya Habari, Sanaa na Utamaduni Pemba inafanya juhudi za kukutana na vijana pamoja na wananchi kwa mambo mawili.
Akitaja mambo hayo, amesema ni pamoja na kuwasisitiza kuvitunza viwanja hivyo na kutoa hamasa kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwa kuonesha vipaji vyao na kujiajiri. Anaeleza kwamba sababu ya kufanya hivyo ni kuondoa dhana potofu katika jamii kuwa mali ya Serikali haipaswi kutunzwa, kumbe sivyo ilivyo.