Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

LIGI KUU: Kuna vita mbili Mbeya

LIGI KUU Pict

Muktasari:

  • Kwenye mechi hizo nane ambazo zote zitachezwa kwa muda mmoja kuanzia saa 10:00 jioni, kila timu itakuwa na hesabu zake ikiwemo kuwania ubingwa na zingine zikipambana kuepuka kuangukia mstari wa kucheza mechi za mtoano ‘play off’ ya kutoshuka daraja.

LIGI Kuu Bara inaendelea leo Jumatano na timu zote 16 zitakuwa kwenye viwanja nane tofauti kusaka hatma ya kutamatisha msimu huu huku kukiwa na mechi moja yenye vita mbili tofauti ikizihusisha Tanzania Prisons dhidi ya Yanga.

Kwenye mechi hizo nane ambazo zote zitachezwa kwa muda mmoja kuanzia saa 10:00 jioni, kila timu itakuwa na hesabu zake ikiwemo kuwania ubingwa na zingine zikipambana kuepuka kuangukia mstari wa kucheza mechi za mtoano ‘play off’ ya kutoshuka daraja.

Katika msimamo wa ligi, Yanga ipo kileleni na pointi 73 ikifuatiwa na Simba (72), kisha Azam (57) na Singida Black Stars (53), huku Tabora United ikikusanya 37.

Zingine pointi zao zipo hivi; JKT Tanzania (35), Dodoma Jiji (34), Mashujaa (33), KMC (33), Coastal Union (31), Namungo (31), Pamba Jiji (30), Tanzania Prisons (30) na Fountain Gate (29). Kagera Sugar (22) na KenGold (16) tayari zimeshuka daraja.


TANZANIA PRISONS VS YANGA

Mbeya kwenye Dimba la Sokoine, Tanzania Prisons itaikaribisha Yanga inayotetea ubingwa wa ligi, kila timu ikiwa na hesabu zake.

Yanga inataka kutetea ubingwa wake ikiwania pointi tatu ili iendelee kusalia juu ya msimamo ambapo sasa inazo 73, wakati Prisons iliyopo nafasi ya 13 na pointi 30, ikitaka kushinda ili iendelee na mapambano yake ya kumaliza ligi sehemu salama.

Katika duru la kwanza, Yanga iliichapa Prisons mabao 4-0 Uwanja wa KMC Complex, Dar.

Kocha wa Yanga Miloud Hamdi akizungumzia mchezo huo, alisema: “Tumekuja Mbeya sio kufanya utalii, tunataka kushinda hii mechi na zingine mbili zitakazofuata ili tufikie malengo yetu, tunafahamu haitakuwa rahisi, tunakutana na timu ngumu Prisons yenye wachezaji washindani,” alisema Hamdi.

kocha wa Prisons, Amani Josiah alisema: “Tupo nafasi ya 13, pointi 30, tumebakiwa na mechi mbili Yanga ambayo inawania ubingwa na sisi tunataka tusicheze mtoano, tutacheza na Singida Black Stars ipo nafasi ya nne kwa pointi 53 inaisaka nafasi ya tatu iliyopo Azam FC yenye alama 57, hivyo utaona ni namna gani tuna mechi ngumu.”


KENGOLD VS SIMBA

KenGold ambayo imeshashuka daraja, itakuwa na dakika 90 za kulinda heshima itakapoikaribisha Simba inayopiga hesabu kali za kuwania taji kuishusha Yanga ambayo ipo juu yao kwenye msimamo. Mchezo huo utapigwa Dimba la Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora huku duru la kwanza Simba ikishinda 2-0.

Simba kupitia Kocha Mkuu, Fadlu Davids akizungumzia mchezo huo, alisema: “Tumejiandaa kukutana na mpinzani mgumu, tulipokutana nao kwenye mechi ya kwanza walicheza vizuri, tunataka kubaki kwenye malengo yetu, tuna wachezaji walio tayari kupigania ushindi.”


AZAM VS TABORA UNITED

Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar, wenyeji Azam wenye pointi 57 nafasi ya tatu, wataikaribisha Tabora United iliyopo nafasi ya tano na pointi 37 huku ikiwa haijashinda mechi tano zilizopita, hii ikionekana kama ni mechi ya kisasi.

Tabora ilishinda 2-1 duru la kwanza, hivyo Azam inataka kulipa kisasi nyumbani huku timu zote zikiwa hazina cha kupoteza kutokana na kutokuwa kwenye nafasi ya kushuka daraja wala kuwania ubingwa.

Kocha wa Azam, Rachid Taousi, alisema: “Tumejiandaa vizuri kukutana na Tabora, hii itakuwa ni mechi yetu ya mwisho nyumbani msimu huu, tunataka mashabiki na viongozi wetu tuwape mchezo mzuri, mapumziko ya ligi yametupa faida kwa wachezaji wote waliokuwa majeruhi kupona, tupo tayari kwa mchezo, tunataka kushinda ili kuongeza pointi zetu kwa kuwa tayari tumeshakata tiketi ya kucheza mashindano ya Afrika ingawa hatukuwa na msimu mzuri.”

Tabora ambayo imengia mjini kimyakimya jana mchana, kocha wao Mzambia Simona Kaunda, alisema: “Tumekuwa kwenye mapumziko kwa muda mrefu, tunajua tunakwenda kukutana na timu ngumu ya Azam, haitakuwa mechi rahisi, kila timu itapigania heshima yake.”


COASTAL VS FOUNTAIN GATE

Coastal Union itakuwa uwanja wa nyumbani wa Mkwakwani jijini Tanga ikiikaribisha Fountain Gate ambapo timu zote zipo kwenye vita ya kukimbia kuangukia mechi za play off.

Endapo Coastal itapata ushindi kwenye mchezo huo, itafikisha pointi 34 ambazo zitaiweka mbali kidogo na pla off wakati wageni wao walioko nafasi ya 14 na pointi 29 wakipoteza tu itakuwa ni kama wamejimaliza na kama wakishinda watajiweka pazuri kidogo.

Kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro akizungumzia mchezo huo, alisema: “Ni mechi ngumu kila timu inapambania nafasi yake, tuna pointi 31, nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu, tukishinda tutasogea juu ingawa itategemeana na matokeo ya timu zingine.”


NAMUNGO VS KAGERA SUGAR

Namungo itakuwa nyumbani Dimba la Majaliwa mkoani Lindi ikijua haipo salama ikihitaji pointi tatu zitakazowafanya kufikisha 34 za kuwatoa kwenye presha ya kucheza play off, inakutana na Kagera Sugar iliyoshuka daraja.

Kocha wa Namungo, Juma Mgunda kuelekea mechi hiyo alisema: “Tumejiandaa kutafuta ushindi, hii ni mechi ambayo inaweza kutupa uhakika wa kukaa nafasi nzuri, wapinzani wetu sio timu mbovu ingawa wamekumbana na matatizo lakini tunajua ugumu wao.”

Juma Kaseja ambaye ni kocha wa Kagera Sugar, alisema: “Tumeshuka daraja lakini haina maana hatuhitaji kufanya vizuri tunatakiwa kuonyesha yaliyotokea sio mambo ambayo yalistahili, tunakwenda kutafuta ushindi.”


DODOMA JIJI VS SINGIDA BS

Pale Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri, wenyeji Dodoma Jiji wataikaribisha Singida Black Stars, hapa zinakwenda kukutana timu mbili zote zitakazowania pointi za heshima.

Wenyeji kama wakishinda mechi hiyo watafikisha pointi 37 wakati Singida iliyokata tiketi ya kucheza mashindano ya Afrika msimu ujao kutokana na kujihakikishia nafasi ya nne, inatafuta kumaliza kwa heshima.


PAMBA JIJI VS JKT TANZANIA

Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kutakuwa na vita ya kufanana, Pamba jiji inahitaji pointi tatu ili itafute salama ya kubaki ligi msimu ujao ikiwa nafasi ya 12 na kama itashinda itafikisha pointi 33.

JKT Tanzania haina presha sana ikiwa nafasi ya sita, kama ikishinda kisha Tabora ikapoteza itafikisha pointi 38 na kukaa nafasi ya tano.

Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix Minziro, alisema: “Hii mechi ni kama fainali kwetu, tumekuwa tunajiandaa kwa muda mrefu tunajua tunakwenda kukutana na moja ya timu bora lakini tutapambana nao.”

Naye kocha wa JKT Tanzania, Hamad Ally, alisema: “Unapokutana na timu kama Pamba Jiji unajua unakutana na timu ngumu, lakini kwa nafasi waliyopo inaongeza ugumu wa mchezo lakini tunataka kushinda ili tupande juu kidogo.”


MASHUJAA VS KMC

Mchezo mwingine utakuwa pale Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma ambapo wenyeji Mashujaa itawakaribisha KMC, hapa zikienda kukutana timu mbili ambazo hazina presha kubwa ya matokeo mabaya.

Mashujaa ambayo ipo nafasi ya nane, chini yao kuna KMC huku zote zikiwa na pointi 33, kama wenyeji watashinda wanaweza kupanda mpaka nafasi ya sita kutegemea na walio juu yao, lakini kama KMC itashinda itaishusha Mashujaa.