Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dar City yabakiza hatua moja kufuzu BAL 2027

Muktasari:

  • Dar City haijapoteza katika michezo yote mitatu iliyocheza, hivyo kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi B, Namuwongo ya Uganda ikimaliza nafasi ya pili.

Dar City imeendelea kuonyesha makali yake katika michuano ya Elite 16 Division East, Road to BAL 2027, baada ya leo Novemba 26, 2026 kuitandika Dolphins ya Botswana kwa pointi 84-61, matokeo yanayoipa timu hiyo nguvu kubwa kuelekea hatua ya nusu fainali, mashindano hayo yanayofanyika Nairobi Kenya.

Dar City haijapoteza katika michezo yote mitatu iliyocheza, hivyo kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi B, Namuwongo ya Uganda ikimaliza nafasi ya pili.

Kwenye mechi hiyo, Dar City ilionyesha ubora katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya ufungaji wa pointi mbili, ambako ilifanikiwa kupata pointi 58 kupitia mikwaju 29 kati ya 43, ikiwa na ufanisi wa asilimia 67.4, huku Dolphins ikifanikiwa kufunga 14 kati ya 45, sawa na asilimia 31.1, jambo lililoonyesha udhaifu iliyokuwa nayo katika kutumia nafasi za karibu.

Katika eneo la mikwaju ya pointi tatu, timu zote zilifunga mikwaju minane, lakini Dar City ilifanya hivyo kupitia majaribio 30, huku Dolphins ikihitaji majaribio 36. Hiyo inaifanya Dar City kuwa na ufanisi wa asilimia 26.7 dhidi ya asilimia 22.2 za Dolphins.

Hata hivyo, Dolphins ilikuwa bora katika mikwaju ya adhabu, ikifunga tisa kati ya 13, sawa na asilimia 69.2, wakati Dar City ilifunga miwili kati ya minne, sawa na asilimia 50.

Takwimu hizo zinaonyesha tofauti kubwa katika mchezo huo ilitokana zaidi na ubora wa Dar City katika kufunga pointi mbili, pamoja na ufanisi wake mkubwa katika kutumia nafasi za kushambulia.

Ushindi huo unaongeza kujiamini kwa kikosi cha Dar City baada ya kufuzu hatua ya nusu fainali na kuonesha benchi la ufundi la timu hiyo wapi kwa kufanyia maboresho ikiwemo matumizi ya mikwaju ya adhabu na kuongeza ufanisi katika mikwaju ya mbali.

Macho yote sasa yanaelekezwa kwenye mchezo unaofuata wa nusu fainali utakaopigwa Novemba 28, 2026 huku ikisubiri kuona timu zipi zitafuzu kutoka kundi A likiundwa na Urunani, Nairobi City, Munali Suns na Patriots BC ambalo linaonekana kuwa na ushindani mkubwa kwani hadi kufikia mechi za mwisho za makundi timu zote zilikuwa na nafasi ya kufuzu nusu fainali.

Mchezo huo utakuwa mtihani wa uwezo, uzoefu na utulivu wa kikosi hicho, kwani hatua za mtoano hazitoi nafasi kubwa ya kufanya makosa.

Ushindi katika mchezo ujao utakuwa hatua muhimu kuelekea lengo la kufuzu BAL 2027 na kuongeza matumaini ya Tanzania kuwa na mwakilishi katika jukwaa kubwa la mpira wa kikapu barani Afrika.

Mfumo wa mashindano unaelekeza timu mbili zitakazomaliza nafasi za kwanza na ya pili katika kila kundi zitafuzu hatua ya nusu fainali itakayochezwa Novemba 28, 2026. Washindi wa nusu fainali watajihakikishia tiketi ya kucheza BAL 2027, huku nafasi nyingine ya kufuzu ikitolewa kwa timu bora iliyomaliza nafasi ya tatu kati ya Division East na Division West.