Last Chance kwa Yanga

Msafara wa timu ya Yanga ulipowasili katika uwanja wa Lubumbashi, Congo juzi Alhamis
Na Michael Momburi, Lubumbashi LUPOPO FC wamekimbia jiji na kujificha, lakini kwa upande mwingine ni nafasi ya mwisho kwa Yanga; Kusonga mbele au kutolewa. hakuna jingine zaidi ya kushinda mabao 2-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga, ambayo jana Ijumaa mchana ilipasha kwenye Uwanja wa Stade de Kenya iko fiti kwa mechi ya leo Jumamosi dhidi ya FC Lupopo na Kocha Kosta Papic amethibitisha. Yanga iliyopiga kambi kwenye Hoteli ya Rose mjini hapa, inashuka uwanjani mchana huu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikihitaji ushindi wa mabao mabao 2-0 kusonga mbele. Katika mchezo wa awali jijini Dar es Salaam, Yanga ilifungwa mabao 3-2, lakini Papic aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa jijini hapa kuwa hana wasiwasi ndio maana yupo hapa. "Mchezo ni mgumu sana, lakini ukweli unabaki pale pale, tumekuja kushinda ndio maana tupo hapa, lolote litakalotokea baada ya mchezo ni mambo ya kawaida,"alisema Papic ambaye waandishi wa televisheni za hapa walionekana kumuogopa kwavile wengi wao hawafahamu Kiingereza zaidi ya Kifaransa na Kilingala. "Kila mmoja nimemuandaa kikamilifu na anajua ni mzigo gani tulionao, tusubiri tuone nini kitatokea, lakini tupo tayari kupigana kwa nguvu zote kutetea hadhi yetu,"alisisitiza huku akisita kutaja kikosi kwa madai angejua baada ya mazoezi ya mwisho ya jioni. Lakini kilichokuwa kikiwaumiza vichwa viongozi wa timu hiyo ni kutopatikana kwa mabegi ya wachezaji; Obren Cuckovic, Boniface Ambani, Godfrey Bonny na Jerry Tegete ambayo yalipotea kwenye mazingira ya kutatanisha Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyata, Nairobi walipokuwa wakibadilisha ndege ya kuja hapa Lubumbashi. "Bado tunahangaika na mabegi yaliyopotea, sijui itakuwaje," Katibu wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Emmanuel Mpangala aliiambia Mwanaspoti mjini hapa. Kwa mujibu wa Obren na Tegete mabegi hayo yalikuwa na vifaa vyao binafsi vya mazoezi vya kuchezea mechi ingawa Meneja Kenneth Mkapa alibeba vingine. Yanga walitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Jommo Kenyatta juzi Alhamisi asubuhi wakiwa na vifaa vyao lakini wakati walipoingia geti namba 4 uwanjani hapo wakaambiwa wasalimishe vifaa vyao na kupewa karatasi maalumu ili wavipokee Lubumbashi, kitu ambacho ni utaratibu wa kawaida kwenye usafiri wa ndege. Lakini walipotua hapa mabegi mengine yakapatikana isipokuwa ya wachezaji hao pamoja na mwandishi wa habari hizi, huku mawakala wa Shirikala Ndege la Kenya (KQ) wakiahidi kushughulikia ingawa kwa mujibu wa wazoefu wa uwanja huo wanadai ni bahati kupata mizigo hiyo. Yanga imekuja hapa ikiwa na muziki kamili pamoja na mwenyekiti wao, Imani Madega.