Kocha Uhamiaji ni suala la muda kutua JKU
Muktasari:
- Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, JKU imemuondosha Kocha Mkuu, Ali Bakari na Msaidizi wake, Hamis Hamad baada ya kutoridhishwa na kiwango cha kikosi hicho.
TIMU ya JKU ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na Kocha Abdulsaleh Mohamed kwa ajili ya kuinoa timu hiyo msimu wa 2026-2027.
Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti kuwa, JKU imemuondosha Kocha Mkuu, Ali Bakari na Msaidizi wake, Hamis Hamad baada ya kutoridhishwa na kiwango cha kikosi hicho.
“Timu ipo katika maandalizi ya msimu wa 2026-2027, hivyo tunahitaji kufanya usajili mzuri kwa ajili ya kukabiliana na ushindani ndiyo maana tunataka kuboresha kwanza benchi la ufundi,” kilisema chanzo hicho.
Akitoa ufafanuzi wa hilo, kocha huyo aliyeiongoza Uhamiaji katika msimu wa 2025-2026, amesema bado wapo katika mazungumzo ya mwisho na mambo yanaendelea vizuri.
“Nipo katika mazungumzo na timu ya JKU lakini bado sijasaini,” amesema kocha huyo.
Wakati huohuo, timu ya Uhamiaji imemuaga kocha huyo kwa kusema: “Tumefikia makubaliano ya kuachana na Kocha Mkuu Abdulsaleh Mohammed. Tunashkuru kwa muda wako wa kuwa nasi katika kipindi chote Cha mapambano.
“Uongozi wa Uhamiaji FC unakushukru kwa jitihada zako za kupambana ili kutoa kile kicho bora kwa timu. Tunakutakia Kila la kheri kwenye safari yako ya mpira.”