Prime
Kocha Simba ataja mbinu za kumaliza mechi mapema
SIMBA imerejea jana jioni ikitokea nchini Malawi, ilipoanza kibabe Ligi ya Mabingwa Afrika, iliposhinda ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Mighty Wanderers, sasa kuna hesabu kutoka kwa kocha wa kikosi hicho, Steve Barker akisema haijaisha na wanautaka ushindi mwingine nyumbani.
Kuelekea mchezo wa marudiano utakaopigwa Septemba 13, 2026 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, sasa itahitaji ushindi au sare yoyote kufuzu hatua ya pili ya mtoano, kutokana na ushindi wa bao la kiungo Anicet Oura kwenye mechi ya mkondo wa kwanza, iliyopigwa juzi Jumapili Uwanja wa Bungu nchini Malawi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesema bado kikosi chake hakijafuzu ambapo wanajipanga kutafuta ushindi mwingine wakiwa nyumbani ili kujihakikishia kwa usahihi tiketi ya kufuzu hatua inayofuata.
Barker amesema licha ya ushindani walioupata kutoka kwa Wanderers, anaamini kikosi chake kitakuwa kwenye ubora tofauti katika mechi ya nyumbani ambayo wataingia na hesabu za kutafuta matokeo mengine mazuri kwa kuwashambulia Wamalawi hao.
“Haikuwa rahisi mechi ya kwanza, tumeifunga timu ambayo ilicheza vizuri, ilitupa ushindani mkubwa, bado hatuna uhakika wa kufuzu, chochote kinaweza kutokea, lakini nini tutafanya ni kujipanga kucheza soka la falsafa yetu kutafuta ushindi mwingine, tukiwa mbele ya mashabiki wetu,” amesema Barker.
“Tutakuwa na mabadiliko kidogo ambayo yatalenga kutafuta ushindi, tunatakiwa kuwa bora katika kuwapa wakati mgumu wapinzani lakini tumalize mechi mapema, hili linawezekana.”
Aidha Barker alionyesha kufurahia kurejea kwa kiungo wake mshambuliaji, Libasse Gueye ambaye atarudi uwanjani baada ya kumaliza adhabu yake ya kutumikia kadi nyekundu akisema, ubora wake utakuwa kitu kingine kigumu kwa Wanderers.
“Ni habari nzuri kwetu kuwa na Libasse, kila mmoja anajua namna alivyouanza msimu huu kwa kasi, anapokuwa uwanjani kuna kitu kikubwa kinaongezeka, tutakuwa na silaha nyingine ambayo naamini itakuwa na faida katika hesabu zetu.”
Gueye alikuwa nje akilazimika kukosa mechi ya mkondo wa kwanza kutokana na kutumikia adhabu hiyo baada ya kuadhibiwa msimu uliopita katika mechi ya ugenini ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola.
Msimu huu Gueye amekuwa na moto akiwa na asisti tano kwenye mechi tano za Ligi Kuu Bara na bao moja, ndiye kinara wa pasi za mwisho.