KMKM yataka makundi CAF
Muktasari:
- Mabingwa hao wa FA watakaoiwakilisha Zanzibar kimataifa, wamesema sasa ni wakati mzuri wa kujipanga dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo wakiweka malengo ya kucheza hatua ya makundi.
MABINGWA wa Kombe la FA Zanzibar, KMKM, wanatarajiwa kuanza mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2026-2027, huku wakilenga kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Mabingwa hao wa FA watakaoiwakilisha Zanzibar kimataifa, wamesema sasa ni wakati mzuri wa kujipanga dhidi ya wapinzani wao katika michuano hiyo wakiweka malengo ya kucheza hatua ya makundi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa KMKM, Ibrahim Khatib Khamis, amesema mapumziko walioyatoa kwa wachezaji yamemalizika, hivyo muda wowote kuanzia sasa wataingia kambini.
“Hadi sasa wachezaji wote wapo vizuri na hakuna taarifa mbaya kuwahusu, wanachosubiria ni taarifa ya kuanza mazoezi,” amesema.
Katika maandalizi hayo wanatarajia kucheza mechi mbalimbali za kirafiki dhidi ya timu kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Amesema, wana mikakati ya kuandaa kikosi imara na kushinda mechi za awali ili kuendelea na hatua nyingine hadi kufika makundi.
“Mipango ni kuvuka hatua ya kwanza kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini zaidi ni kucheza makundi ili kuweka rekodi mpya na sio kuishia tena hatua ya pili.”