Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipute Ligi Kuu hakuna kulala

Muktasari:

  • Kagera Sugar itakayokuwa Uwanja wa Kaitaba, uliopo Manispaa ya Bukoba, Mkoa wa Kagera, imecheza mechi nne za Ligi Kuu Bara mfululizo bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoichapa Mbeya City mabao 3-1, ikiwa ugenini, Oktoba 9, 2026.

LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo kwa mechi mbili kupigwa kwenye viwanja mbalimbali na Kagera Sugar itaikaribisha TRA United saa 12:00 jioni, huku Geita Gold ikiwa nyumbani dhidi ya maafande wa Mashujaa FC kuanzia saa 2:30 usiku.

Kagera Sugar itakayokuwa Uwanja wa Kaitaba, uliopo Manispaa ya Bukoba, Mkoa wa Kagera, imecheza mechi nne za Ligi Kuu Bara mfululizo bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoichapa Mbeya City mabao 3-1, ikiwa ugenini, Oktoba 9, 2026.

Katika mechi nne, Kagera Sugar imetoka sare moja na kuchapwa tatu mfululizo ikiwa haina mwenendo mzuri hadi sasa, baada ya kushinda moja, sare tatu na kupoteza saba kati ya 11, iliyocheza, ikiburuza mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi sita.

Kwa upande wa TRA United ina kumbukumbu nzuri baada ya mechi yake ya mwisho kuifunga Fountain Gate mabao 3-2, Novemba 2, 2026, ikiwa ni ushindi wa pili kati ya 10, ikitoa sare tano na kupoteza mitatu, ikishika nafasi ya 12 na pointi zake 11.

Mechi ya mwisho leo, itapigwa kwenye Uwanja wa Bukombe uliopo mji mdogo wa Ushirombo, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita na wenyeji, Geita Gold itakuwa na kibarua kingine kigumu saa 2:30 usiku, kwa kuwakaribisha maafande wa Mashujaa FC.

Geita Gold imekuwa na mwenendo usioridhisha hadi sasa katika Ligi Kuu Bara, baada ya kucheza mechi nane mfululizo bila ushindi, tangu mara ya mwisho kikosi hicho kilipoibuka na ushindi wa mabao 6-2, dhidi ya Kagera Sugar, Agosti 22, 2026.

Mwenendo huo wa Geita Gold, umeifanya timu hiyo kushinda mechi mbili tu kati ya 11, iliyocheza hadi sasa, ikitoka sare tatu na kupoteza sita, ikiwa nafasi ya 13 na pointi tisa, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 11 na kuruhusu 18.

Kwa upande wa Mashujaa FC, inaingia na kumbukumbu nzuri baada ya mechi ya mwisho kabla ya kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuifunga Pamba Jiji kwa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Novemba 2, 2026.

Katika mechi 10, ilizocheza kikosi hicho cha maafande kwa msimu huu wa 2026-2027, kimeshinda tano na kupoteza pia tano, ikiwa nafasi ya tisa na pointi 15, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 15.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara, ilikuwa Februari 25, 2024, ambapo Mashujaa ilishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na Adam Adam, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ na David Ulomi, huku la Geita Gold likifungwa na Tariq Seif Kiakala.

Kocha Mkuu wa Geita Gold, Zubery Katwila alisema baada ya mapumziko mafupi amepata nafasi ya kukaa na kuzungumza zaidi na wachezaji wa kikosi hicho, huku mazungumzo hayo yakiwa ni ya kuwajenga kisaikolojia ili kurejesha morali tena upya.

“Matokeo mabaya yanashusha morali ya timu ingawa, tumekaa na kuwajenga wachezaji kisaikolojia ili kurejea katika hali yao ya kujiamini, tunakutana na Mashujaa FC iliyoimarika zaidi ila tutapambana kubaki na pointi tatu,” alisema Katwila.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Amani Josiah alisema licha ya mwenendo wa wapinzani wao, ila anatarajia mechi hiyo itakuwa ni ngumu kutokana na mahitaji ya kila mmoja, huku akiwataka wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa nidhamu.