Kilio cha watanzania na maono ya Poulsen kwa Samatta
Muktasari:
Kocha huyo aliyefahamika hapa nchini kama babu, alisema alimuacha Samatta kwa sababu hakuwa akijitoa kwa ajili ya Stars...hajitumi!
Februari 2012, Kocha wa Taifa Stars Mdenishi, Jan Poulsen alitangaza kikosi cha kuivaa Msumbiji kufuzu AFCON 2013.
Lakini kabla ya mchezo huo, kukawa na mchezo wa kirafiki dhidi ya DRC. Michezo yote ilipangwa kufanyika hapa hapa nyumbani.
Poulsen akamuacha Mbwana Samatta na kumuita John Bocco kama mshambuliaji pekee.
Kocha huyo aliyefahamika hapa nchini kama babu, alisema alimuacha Samatta kwa sababu hakuwa akijitoa kwa ajili ya Stars...hajitumi!
Wakaja DRC, mechi ikaisha 0-0. Wakaja Msumbiji, mechi ikaisha 1-1.
Katika mechi zote hizo, babu alimwamini John Bocco, akisaidiwa na Vincent Barnabas aliyekuwa akitokea pembeni na Abdi Kassim ambaye alikuwa nyuma kama mshambuliaji wa pili.
Kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi dhidi ya Msumbiji, Poulsen alibanwa na waandishi juu ya kwanini hakumuita Samatta.
Mzee wa watu akatetea uamuzi wake akitumia maneno ya Kiingereza, ‘He’s not a team player’, na ‘He’s not commited’.
Kila akijibu swali moja, linalofuata ni lilelile...kwanini umemuacha Samatta. Babu akasusa na kutoka kwenye chumba cha mkutano na kuwaacha waandishi wakiwa peke yao.
Wachambuzi wakamjia juu sana kocha huyo wakisema anaihujumu timu kwa kumuacha mshambuliaji pekee tegemeo wa Tanzania.
Lakini babu aliendelea kusisitiza, Samatta hajitumi!
Mei mwaka huo babu akafungashiwa virago vyake na TFF...akaondoka!
Mdenishi mwenzake, Kim Poulsen, aliyekuwa kocha wa timu ya vijana, akapandishwa na kukabidhiwa Stars.
Akamuita Samatta kwenye kikosi chake cha kwanza kabisa, kilichotakiwa kuikabili Ivory Coast ugenini.
Akaendelea naye lakini kufika Desemba 2013 akamtumbukia nyongo.
Ilikuwa wakati wa kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Afrika, Zambia.
Kim aliita kikosi cha wachezaji 24, wakiwemo Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe.
TFF ikatuma tiketi za ndege hadi DRC ili wachezaji hao waje...na kweli wakaja lakini hawakuripoti kwenye kambi ya Taifa Stars.
Siku ya mechi wakaja wote wawili uwanjani wakiwa wamevaa ‘headphones’ zao masikioni, wakitokea majumbani kwao.
Mtangazaji wa uwanjani, akawatambulisha kwamba wapo uwanjani na wakaombwa kusimama kuwasalimia Watanzania...uwanja mzima ukaanza kuwazomea kwa kuigomea Stars.
Shabiki mmoja alishika bango lililoandikwa, ‘Who Needs Samatta, We’ve Got Ngassa’.
Na kweli, Mrisho Ngassa akafunga bao pekee na la ushindi kwa Stars, dhidi ya Mabingwa wa Afrika ambao walikuwa wakielekea Afrika Kusini kutetea ubingwa wao.
Baada ya mechi, beki wa Zambia, Stopila Sunzu, ambaye alikuwa akicheza TP Mazembe na kina Samatta, alishangaa kutowaona kwa sababu alitarajia kukutana nao.
Alisema hakuwa na taarifa yoyote kwamba walikuwa majeruhi, hivyo haelewi kwanini hawakuwepo.
Kocha wa Stars, Kim Poulsen, akioneshaa kukerwa, akasema hatamuita tena mchezaji yoyote asiyeonesha mapenzi kwa timu.
Maisha yameendelea na sasa ni miaka takribani minane imepita na Samatta ndiyo nahodha wa Taifa Stars.
Amekuwa mkubwa kiasi hakuna kocha anayeweza kuthubutu kutomuita, kama alivyofanya babu Jan Poulsen. Au hata kumsema tu, kama alivyofanya Kim Poulsen.
Samatta anafanya masihara na roho za watu. Mechi muhimu ya kufuzu dhidi ya Cape Verde, anapiga penalti ya ‘kideoni’ anakosa na kuwaweka watu roho juu...halafu anacheka.
Mechi dhidi ya Burundi kufuzu Kombe la Dunia, kuna mtu alikufa uwanjani baada ya Samatta kukosa goli.
Samatta anazurura uwanjani kiasi cha kuzidiwa hata na Ditram Nchimbi, kwenye kupambana uwanjani.
Ndiyo maana Watanzania wameamua kusema wenyewe kwa kupata sauti zao.
Watu wamekiona kile alichokiona Mdenishi wa watu, miaka mingi iliyopita...kwamba Samatta hachezi kwa ajili ya timu (He’s not a team player) na hajitoi kwa ajili ya timu (he’s not committed).
Wale waandishi waliokuwepo siku ile kwenye mkutano wa habari wa Jan Poulsen, baada ya mechi dhidi ya Msumbuji, ambao wachache wao bado wapo, hawasimami na kutoa ushahidi kwamba Samatta alionesha tabia hizi tangu zamani.
Watanzania wamevumilia siku nyingi, sasa wameamua kulipuka na kusema.
Siyo kwamba hawampendi Samatta...wanampenda sana. Wanafuatilia Ligi ya Ubelgiji sababu yake. Lakini kipigo cha 2-1 dhidi ya Libya ndicho kilichowatibua.
Mipira mingi ilipotelea kwake, halafu hakabi...anacheka tu!
Wenzake wanapambana kukaba, halafu wanampasia...anapoteza, anacheka.
Watu wanaona, ufahamu wao kuhusu mpira umekuwa mkubwa...ndiyo maana wanalalamika.
Mechi ijayo ya AFCON tutacheza na Tunisia, Agosti 2020. Hofu uyangu isije kuwa Watanzania wakaanza kuzomea siku ya mechi na kuwavunja moyo wachezaji wengine.
Mungu Ibariki Tanzania!