Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilimanjaro Wonders Queens yaonja pointi ya kwanza baada ya dakika 270

Muktasari:

  • Matokeo hayo yaliyopatikana leo Novemba 11, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro, yamehitimisha mwanzo mgumu wa timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu, baada ya kupoteza michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba Queens na Mashujaa Queens.

Kilimanjaro Wonders Queens imepata pointi yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara  baada ya kusubiri kwa dakika 270 sawa na michezo mitatu, kufuatia kutoka sare ya 0-0 na Fountain Gate Princess.

Matokeo hayo yaliyopatikana leo Novemba 11, 2026 kwenye Uwanja wa Ushirika uliopo Moshi mkoani Kilimanjaro, yamehitimisha mwanzo mgumu wa timu hiyo iliyopanda daraja msimu huu, baada ya kupoteza michezo miwili iliyopita dhidi ya Simba Queens na Mashujaa Queens.

Katika mchezo wake wa kwanza, Kilimanjaro  Wonders Queens ililala kwa mabao 3-0 dhidi ya Simba Queens, kabla ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mashujaa Queens.

Hata hivyo, dhidi ya Fountain Gate Princess, timu hiyo imeonekana kuimarika katika safu ya ulinzi na kuzuia wapinzani wasipate bao, ingawa nayo imeshindwa kutumia nafasi ilizozipata kutikisa nyavu.

Kwa upande mwingine, Fountain Gate Princess pia iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya vipigo viwili, ikifungwa mabao 3-1 na Mashujaa Queens kabla ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba Queens.

Baada ya matokeo hayo, timu zote zimefikisha pointi moja katika michezo mitatu, zikiwa na sare moja na vipigo viwili kila moja.

Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Kilimanjaro Wonders Queens, Daudi Macha, amesema pointi hiyo ina thamani kwao kutokana na uzoefu wa Fountain Gate Princess katika ligi hiyo.

Amesema kikosi chake kinajengwa kwa wachezaji wengi waliopandishwa kutoka daraja la chini, hivyo michezo hiyo imekuwa sehemu ya kujifunza na kuzoea ushindani wa ligi.

Macha amesema lengo la timu hiyo msimu huu ni kumaliza ndani ya nne bora, huku akieleza sare hiyo imeongeza kujiamini kwa wachezaji kuelekea michezo ijayo.

"Ukiangalia mechi na Simba, makosa yaliyotokea siyo yale yaliyotokea dhidi ya Mashujaa. Hata makosa ya leo siyo yatakayojirudia dhidi ya Yanga, kwa sababu kila siku tunarudi uwanjani kurekebisha," amesema.

Ameongeza kuwa, Kilimanjaro Wonders Queens haijaanza msimu kwa lengo la kugombea ubingwa, bali wanataka kujenga timu itakayoweza kushindana na kumaliza katika nafasi nne za juu, akiahidi kuwapa wananchi wa Kilimanjaro kitu cha kushangaza msimu huu.

Kwa upande wa Fountain Gate Princess, kocha wake Luhaga Makunja, amesema licha ya kupata sare ugenini, timu imeonyesha maendeleo, lakini bado wana kazi ya kuboresha umaliziaji wa nafasi za kufunga.

Makunja amesema walitengeneza nafasi kadhaa dhidi ya Kilimanjaro Wonders Queens, lakini wachezaji walishindwa kuzitumia, akieleza kuwa watarejea uwanjani kwa ajili ya kurekebisha changamoto hiyo.

"Leo tumekuja ugenini na kupata clean sheet, lakini kitu kikubwa ni kwamba tumetengeneza nafasi na kushindwa kuzibadilisha kuwa mabao. Kutengeneza nafasi ni kitu kingine, lakini kuzimalizia ni kitu kingine," amesema Makunja.

Amesema maandalizi ya mchezo huo yalikuwa na changamoto kutokana na kutokuwa na taarifa nyingi kuhusu Kilimanjaro Wonders Queens ambao ni wageni katika ligi hiyo, lakini alisifu namna timu hiyo ilivyocheza kwa kujilinda na kutumia mashambulizi ya kushtukiza.

Naye Ofisa Habari na Mawasiliano wa Fountain Gate Princess, Issa Liponda maarufu Issa Mbuzi, amesema pointi moja waliyoipata haikuwa lengo lao, kwani walikuwa wameifuata Kilimanjaro Wonders Queens kwa dhamira ya kuondoka na pointi zote tatu.

Mbuzi amesema timu yao ilitengeneza nafasi za kutosha kushinda, lakini ilikwamishwa na uimara wa safu ya ulinzi ya wenyeji, akiwataja Sifati Kasindo na Mwajabu Athumani kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya kazi kubwa kuzuia mashambulizi yao.

Amesema sare hiyo ni hatua ya kuimarika kwa timu yao baada ya kupoteza michezo miwili ya iliyopita, lakini akasisitiza hawataridhika na matokeo hayo kwa kuwa bado wana kazi ya kujenga kikosi chenye ushindani katika ligi hiyo.