Kigwangala aukataa uenyekiti Simba akitaja uwekezaji
Muktasari:
- Kauli ya Kigwangall imekuja baada ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kulitaja jina lake kuwa miongoni mwa Wanachama wa Klabu hiyo wanaohusishwa na kuwania nafasi hiyo.
Aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla amesema hana mpango wa kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Klabu ya Simba katika Uchaguzi wake Mkuu utakaofanyika Januari 30, 2026.
Kauli ya Kigwangall imekuja baada ya baadhi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kulitaja jina lake kuwa miongoni mwa Wanachama wa Klabu hiyo wanaohusishwa na kuwania nafasi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dk Kigwangalla amesema kuwa ndoto zake ni kumiliki hisa za klabu hiyo.
“Watu wengi wamekuwa wakinitafuta na kunihamasisha nichukue uongozi wa Simba Sports Club. Naona hata ‘media’ zimeanza kuniandika, huku kukiwa na baadhi ya ‘comments’ za kejeli. Kwanza, narudia kuwashukuru sana kwa imani hiyo. Lakini nirudie nilichokwisha kusema. Sina mpango wa kugombea nafasi yoyote ya uongozi Simba wala popote pale kwa sasa.
“Kwa upande wa Simba, ningependa zaidi kuwa mwekezaji kwa kununua hisa za klabu,” amesema Kigwangalla.
Kigwangalla amesema kuwa kwa sasa amejipa muda wa kujitafakari na kusimamia mambo yake binafsi.
“Zilitokea fursa za kugombea Ubunge wa Afrika Mashariki. Waheshimiwa wabunge wengi walinihamasisha niende, wengine wakajitolea hata kunisaidia kampeni. Niliwashukuru kwa heshima hiyo, lakini sikuona sababu ya kugombea.
“Nyumbani Tabora nako, kumekuwa na watu wanaonihamasisha nijipange kuchukua nafasi za uongozi ndani ya chama mkoani. Hata huko sijaitikia. Siyo kwamba siwezi, sipendi au sina sifa. La hasha!
“Bado natafakari sana kuhusu maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine dhidi ya kutumia muda na nguvu kujenga urithi kwa ajili ya familia yangu, hasa wajukuu zangu. Kuna watu wanaamini kwamba kushika nafasi ya uongozi wa umma, chama au taasisi ni fursa ya kujitengenezea fedha. Pengine kwa baadhi ni hivyo.
“Lakini kwa wengi, ukweli ni tofauti. Ni kujitoa, kujitolea na kutumia muda na nguvu kujenga cha wote, wakati mwingine kwa gharama ya kuchelewesha kujenga cha kwako na cha familia yako,” amesema Kigwangalla.
Katika Uchaguzi huo wa Simba, nafasi zitakazogombewa ni moja ya Uenyekiti na tano za wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.