Kigogo Yanga: Kwa usajili huu kuna timu itafungwa 10
Muktasari:
- Yanga katika maboresho ya kikosi chake, imesajili wachezaji wapya 14, wakiwemo saba wa kimataifa na wazawa saba.
KIWANGO cha kikosi cha Yanga msimu huu ilichoanza kukionesha hakiwafurahishi tu mashabiki, bali hadi viongozi wa klabu hiyo nao wanachekelea, huku kigogo mmoja akiweka wazi kwamba kuna timu itakuja kufungwa mabao 10.
Yanga katika maboresho ya kikosi chake, imesajili wachezaji wapya 14, wakiwemo saba wa kimataifa na wazawa saba.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, amesema usajili ambao wameufanya umeanza kutoa picha halisi ya msimu utakavyokuwa.
"Nipongeze uongozi kwa ujumla hasa kwenye hesabu za usajili kuna kazi kubwa imefanyika ya kusajili wachezaji ambao wanatoa mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho pamoja na kocha," amesema kigogo huyo.
Arafat amesema benchi la ufundi la Yanga limeendelea kufanya kazi kubwa ya kusuka timu hiyo yenye wachezaji mchanganyiko wa zamani na wapya.
"Benchi la ufundi limefanya kazi kubwa inayotoa mwanga mkubwa kwa kiwango ambacho kinaonekana sasa kinatupa nguvu kama viongozi kuna malengo yale tuliyojiwekea yakitimia.
"Msimu huu kuna uwezekano mkubwa wa timu yetu kucheza kwa ubora zaidi na kuwa tishio kwenye ligi. Naamini kuna timu inaweza kufungwa hata mabao 10 kutokana na nafasi nyingi zinazotengenezwa na zinazotumika," amesema Arafat.
Yanga mpaka sasa imecheza mechi tatu za Ligi Kuu Bara ikiwa haina rekodi kupoteza mchezo hata mmoja, ikifunga mabao 11 na kuruhusu mawili ikizifunga Namungo (3-1), Coastal Union (4-1) na JKT Tanzania (4-0).
Yanga imefanya usajili kwenye maeneo yote msimu huu, huku ikichukua wachezaji wakigeni na wenyeji ambapo jumla yake ni 13.
Wachezaji hao upande wa kimataifa ni Peter Shalulile (mshambuliaji raia wa Namibia), Albert Kangwanda (mshambuliaji raia wa Zambia), Cheikh Touré (mshambuliaji raia wa Ufaransa), Housseine Zakouani (winga raia wa Comoros), Farouk Oumar Komara (beki raia wa Ivory Coast), Fred Duval Ngoma (kiungo mkabaji raia DR Congo) na Stephanie Aziz KI (kiungo raia wa Burkina Faso).
Wazawa ni Erick Mwijage (winga), Mohamed Mussa (beki), Hussein Mihambo (mshambuliaji), Juma Issa Abushiri “Chuga Boy” (winga), Abdulnasir Mohamed “Gamal” (beki wa kulia), Suleiman Mbarouk (winga) na Seleman Mwalimu (mshambuliaji).
Katika mechi tatu ilizocheza Yanga, imeshinda zote ikizifunga Namungo (3-1), Coastal Union (4-1) na JKT Tanzania (4-0), huku nyota wapya waliofunga ni Albert Kangwanda mwenye mabao mawili na asisti moja, Peter Shalulile (mabao mawili), huku Housseine Zakouani akiwa na asisti tatu.