Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kigogo Madini United aichorea ramani Ligi Kuu

MADINI Pict

Muktasari:

  • Timu hiyo yenye makazi yake Kahama mkoani Shinyanga, inatajwa kuwa yenye ushawishi na nguvu kubwa ya wadau na mashabiki wakiitabiria kuongeza chachu kwenye soka Kanda ya Ziwa.

BAADA ya kuanza kwa ushindi katika First League, uongozi wa Madini FC umetamba kuwa kiu yao ni kuona wanafika Ligi Kuu kutokana na mipango waliyonayo na ndoto za mafanikio kwenye medani za soka.

Timu hiyo yenye makazi yake Kahama mkoani Shinyanga, inatajwa kuwa yenye ushawishi na nguvu kubwa ya wadau na mashabiki wakiitabiria kuongeza chachu kwenye soka Kanda ya Ziwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Madini United, Mhandisi Geneya Geneya, amesema baada ya kuanzishwa kwa chama hilo, malengo na mkakati ni kuona wanaifikia Ligi Kuu miaka miwili ijayo, akiomba wadau na mashabiki kuendelea kuisapoti.

Amesema usajili walioufanya wa wachezaji mchanganyiko ni hatua ya kwanza kusaka mafanikio kwenye soka, akiahidi kuwa wanahitaji kuona Kanda ya Ziwa ikiongeza timu za Ligi Kuu.

“Timu yetu imesajiliwa rasmi 2023, japokuwa tulianza kama kikundi cha mazoezi ‘Jogging’ tukaona upo umuhimu wa kuiweka kwenye soka la ushindani, tukacheza Ligi ya Mkoa na kutwaa ubingwa, RCL tukafanya vizuri hadi kupanda First League.

“Ushindi wa mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Alliance ni matunda tuliyowekeza kwakuwa tumesajili vizuri na tunao ushirikiano wa wadau na mashabiki kila mmoja anatamani kuona Kahama inakuwa na Ligi Kuu,” amesema Geneya.

Kigogo huyo ameongeza kuwa, pamoja na mipango waliyonayo hawawezi kudharau timu pinzani walizonazo kwenye kundi badala yake kila mchezo kwao ni kuhakikisha wanashinda ili kufikia malengo.

First League ilianza kutimua vumbi juzi kwa mechi tatu kupigwa viwanja tofauti, ambapo Madini United ikiwa ugenini jijini Mwanza iliichakaza Alliance mabao 4-2 na mchezo ujao itarejea Nyamagana jijini humo kukipiga na Copco katika kundi B.

Kigoma FC nayo ya kundi B ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mt Hanang na kuanza matumaini mapya ya kuisaka Championship msimu ujao na hatimaye kuifukuzia Ligi Kuu.

Hausung ya mkoani Njombe iliyoshuka daraja msimu uliopita kutoka Championship, ilianza vyema pia kwa kuicharaza Barberian ambayo ilishuka daraja kwa bao 1-0 na kuwa kileleni mwa muda kundi A ikisubiri matokeo ya timu nyingine.