Kigogo Ceassia Queens afunguka
Muktasari:
- Ceassia Queens, ambayo imedumu Ligi Kuu ya Wanawake kwa misimu mitano mfululizo, ilianza msimu kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Alliance Girls katika mchezo uliochezwa nyumbani mkoani Iringa.
LICHA ya kuanza kwa kipigo katika Ligi Kuu ya Wanawake Bara (WPL), Ceassia Queens imesisitiza kuwa haijapoteza mwelekeo wa malengo yake ya kumaliza msimu huu katika nafasi nne za juu.
Hata hivyo, timu hiyo imekiri kuwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya kikosini msimu huu, hasa uamuzi wa kutegemea wachezaji wazawa pekee, yanaweza kuleta changamoto katika kujenga muunganiko wa timu.
Ceassia Queens, ambayo imedumu Ligi Kuu ya Wanawake kwa misimu mitano mfululizo, ilianza msimu kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Alliance Girls katika mchezo uliochezwa nyumbani mkoani Iringa.
Sasa timu hiyo inajiandaa kukabiliana na Bunda Queens, inayotajwa kuwa miongoni mwa timu zinazofanya vizuri katika ligi hiyo.
Ceassia Queens ndiyo mwakilishi pekee wa ukanda wa Nyanda za Juu Kusini katika ligi hiyo, huku ikiwa imeendelea kuwa sehemu muhimu ya burudani ya soka kwa wadau na mashabiki mkoani Iringa tangu Lipuli FC iliposhuka daraja.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Jumanne Joseph, amesema kipigo cha mchezo wa kwanza kilichangiwa na maandalizi yasiyoridhisha, lakini kwa sasa kikosi kimejipanga kurekebisha makosa na kupambana kupata ushindi katika mchezo ujao.
Amesema licha ya kuwa na lengo la kumaliza nafasi nne za juu, mabadiliko makubwa ya wachezaji yanaweza kuathiri kasi ya timu katika hatua za mwanzo za ligi.
“Msimu huu tumefanya mabadiliko makubwa. Awali tulikuwa na wachezaji mchanganyiko, wakiwamo wa kimataifa, lakini sasa wote ni wazawa. Pia tumeongeza wachezaji wapya 16 kati ya 26 waliopo kikosini,” amesema na kuongeza:
“Hali hiyo inaweza kutupa ugumu kwa sababu tunahitaji muda kujenga muunganiko wa timu. Hata hivyo, kwa namna vijana wanavyoonyesha uwezo wao, tunaamini tunaweza kupambana na kufikia malengo yetu ya kumaliza katika nafasi nne za juu. Kipigo cha juzi hakijatutoa kwenye hesabu zetu.”
Jumanne amesema Ceassia Queens ina wajibu mkubwa kwa mashabiki wa soka wa Iringa, hivyo wataendelea kupambana kuhakikisha timu hiyo inatoa burudani na kufanya vizuri katika ligi.