Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Khadija Kopa afunguka kuhusishwa kifo cha Leila Khatibu, mwanaye Omar

Muktasari:

Kopa alishirikishwa na msanii wa Bongo Fleva, Isihaka Nassor ‘Aslay’, katika wimbo wake wa “Usiitie doa”.
Pia, amepata kushirikiana na waimbaji wengine wa kike kama vile Mwanamtama Amir, Leila Khatib (marehemu) na wanaume kama akina Abdul Misambano na Ali Star ‘Sharo Babu’.

“UMAARUFU kwa wasanii ni mzuri na unarahisisha baadhi ya mambo, lakini wakati mwingine unaleta madhara makubwa sana. Utazushiwa mambo ya uwongo ili uchafuke tu.
“Niliwahi kuzushiwa kuwa nilimuua mwanangu Omar Kopa, eti nijiongezee umaarufu baada ya kuonekana nimeanza kupotea.
“Hata Leila Khatib alipofariki, niliambiwa kwamba mimi ndiye niliyemuua”alizungumza kwa uchungu Khadija Kopa.
Uzushi huo ukakuzwa zaidi wakati wa mazishi ya Leita, ambapo Khadija hakudhuria kutokana na yeye pia kufiwa na bibi yake hivyo, waliotengeneza jungu hilo wakapata nguvu zaidi ya kusambaza.
“Hapa kwetu ukiwa msanii mzuri na Mungu kakujali kipaji basi unageuzwa kuwa malaika mtoa roho. Msanii mwenzako akiumwa, unaogopa hata kwenda kumuangalia,” aliongeza Khadija, wakati akianza mazungumzo yake na mwandishi wetu kuhusiana na masuala mbalimbali juu ya muziki wa taarabu na maisha yake kwa ujumla.

IMETOKEA WAPI
SIFA za msanii wa muziki wa taarab Khadija Omar Kopa, zimezagaa kila kona katika nchi zilizo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na Falme za Kiarabu.
Ana uwezo mkubwa wa kutunga, kuimba na utayarishaji wa rekodi nyimbo za taarab pia ni mfanyabiashara na kada maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Khadija amejizolea sifa lukuki kwa kuimba nyimbo zenye mipasho, inayopendwa na wapenzi na washabiki wa muziki wa taarab humu nchini.
Amekusanya mashabiki kila kona kutokana na ubora wa kazi zake, yaani nadra sana kwa malkia huyu wa taarabu kuachia ngoma kisha isiwabambe mashabiki.
Khadija alizaliwa 1963 huko Zanzibar, alipewa jina la Khadija akiwa ni mtoto wa kipekee katika familia ya Omar Abdallah Kopa.

Alivyojiunga Culture Musical Club.
Khadija amebeba historia ya maisha yenye kuvutia sana kwenye muziki wa taarabu. Anakumbuka siku moja alikuwa amekaa nyumbani kwao huku akiiga kuimba wimbo, akapita babu yake aliyekuwa katika kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar.
Babu huyo akamsifia ya kwamba, anajuwa kuimba na baada ya sifa hizo, Khadija akajiona anatosha kujiunga katika kundi kubwa la muziki huo.
Akachukuwa hatua ya kuandika barua pasipo kumshauri babu yake, akaipeleka kwenye uongozi wa Culture Musical Club akiomba ajiunge nao.
Alikubaliwa na kuweza kuanza fanya kazi ya kuimba nyimbo za taarab tangu mwaka 1990, katika kundi lake hilo.
Wakati akiwa Culture Musical Club, kipaji chake kilionekana mapema baada ya kuimbaji kwa mahiri mkubwa kupitia sauti yake maridhawa.
Khadija aliimba vibao vya kama vile “Kadandie”, “Daktari” na “Wahoi”, akiwa Culture Musical Club, ambavyo vilimpa umaarufu mkubwa visiwani Zanzibar na Pemba.
Sifa zake zikatambaa hadi Tanzania Bara, ambako uongozi wa Tanzania One Theatre Plus (TOT), ulifanya mchakato wa kumfuata Khadija, wakamuomba ajiunge na kikundi hicho.
Sababu kubwa ilikuwa ni kukipa sura na mwonekano mpya, tofauti na tasnia ya taarab iliyozoweleka Tanzania Bara.
Khadija aliamua kuhamia jijini Dar es Salaam baada ya kushawishiwa na uongozi wa TOT kujiunga nacho, wakati huo  kikiongozwa na Kapteni mstaafu John Damian Komba mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Awali, baadhi ya washabiki wa muziki huo hususan katika jiji la Dar es Salaam, hawakuwa wakifahamu uwezo wake katika kuimba. Waliomuona kama mwimbaji wa kawaida, tofauti na mashabiki wa taarab wa visiwa vya Zanzibar, jina la Khadija Kopa lilikuwa kubwa mno.
Licha ya kuimba taarab, amekuwa mstari mbele katika uimbaji wa kwaya ya TOT, akishirikiana vyema na Kapteni Komba (marehemu) pamoja na waimbaji wengine wa TOT wakiwamo akina Abdull Misambano, Mwanamtama Amir na wengine wa kundi hilo.
Khadija hujichanganya kupiga muziki na baadhi ya bendi za muziki wa dansi na Bongo Fleva, humualika kuongeza sauti yake yenye mvuto kwenye nyimbo zao.
Mfano wa karibu ni pale aliposhirikiana vyema na wanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu, wakatengeneza video ya wimbo wa ‘Chanzo ni Wanaume’. Khadija ameonekana akiimba kwa kupokezana na waimbaji wa bendi hiyo Jose Mara na Kharid Chokoraa.
Aidha, aliwahi kushirikiana na msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, aliyekuwa kiongozi wa kundi la taarab la Jahazi, Alhaj Mzee Yusuph.
Kopa alishirikishwa na msanii wa Bongo Fleva, Isihaka Nassor ‘Aslay’, katika wimbo wake wa “Usiitie doa”.
Pia, amepata kushirikiana na waimbaji wengine wa kike kama vile Mwanamtama Amir, Leila Khatib (marehemu) na wanaume kama akina Abdul Misambano na Ali Star ‘Sharo Babu’.
Waliporomosha nyimbo ambazo zilitamba miaka hiyo kupitia mashairi maridadi yaliyotungwa na kuimbwa na nguli hao.
Khadija ni mama mwenye watoto wanne na wajukuu wawili, pia hujishughulisha masuala ya siasa ambapo aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa ya CCM (NEC).
Ndio kwanzaa utamu wa malkia huyu wa taarabu umeanza, endelea kufuatilia simulizi yake ambapo, amefichua mambo mengi. Unajua nini kuhusiana na mumewe, mtoto wake Omar Kopa na mikasa aliyopitia kwenye taarabu. Unajua ndoto yake na mwanaume gani alimficha ndani ya moyo wake? Fuatilia kesho Jumatatu.