Kaseja anaendelea kutupa somo la kujifunza
Muktasari:
Kaseja alipotea katika soka la Tanzania baada ya kucheza kwa mafanikio Simba, Yanga na Taifa Stars jambo ambalo mashabiki wengi wa soka nchini walifikia hatua ya kumstaafisha na hata kumuita mzee na anatakiwa kuachana na maisha yenyewe ya soka.
MWEZI wa Agosti mwaka huu umekuwa na matukio mengi hasa katika upande wa soka kwenye timu za taifa na hata klabu, kwa kuweka rekodi mbalimbali na matukio ambayo yameendelea kufanyika ambayo kwa namna moja au nyingine yameendelea kuwa alama katika mchezo huu.
Katika matukio ya klabu kulikuwa na Wiki ya Mwananchi ambayo ilihitimishwa Agosti 4, ambapo kikosi cha Yanga kilicheza mechi ya kirafiki na timu ya Kariobang Sharks ya Kenya - pambano ambalo lilimalizika kwa sare.
Simba nao, kama kawaida walihitimisha Simba Day jana, Agosti 6, baada ya kucheza mechi ya kirafiki na timu ya Power Dynamos kutokea Kitwe, Zambia na kuweka rekodi ya kutimiza Simba Day ya kumi tangu kuanzishwa kwake.
Simba na Yanga katika wiki zao kabla ya hitimisho walikuwa na matukio mengi mbalimbali kama kufanya usafi, kuzindua jezi, viwanja, kuingia mikataba na baadhi ya wadhamini na mambo mengine mengi ambayo yote kiujumla yaliweka alama katika soka hasa mwezi huu wa Agosti.
Ukiachana na matukio hayo ambayo wameyafanya Simba na Yanga, timu za Taifa mbili - kwa maana ile ya wanawake iliyokuwa katika mashindano ya Cosafa kule Afrika Kusini imeweka rekodi ya kutinga hatua ya nusu fainali huku wakiwa wanatoa vipigo vya maana. Pia Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Kwa Taifa Stars hapa ndipo kuna somo kubwa la kujifunza baada ya kutinga hatua ya pili katika fainali za kufuzu Chan ambazo zitafanyika nchini Cameroon ambapo watacheza na timu ya Taifa ya Sudan.
Stars kushinda dhidi ya Kenya ugenini kwa penati 4-1, na hata kama itapata nafasi ya kufuzu Chan, linaweza lisiwe jambo kubwa kama ambavyo kazi ya mlinda mlango Juma Kaseja aliyoifanya katika mechi zote mbili - ya hapa nyumbani na ugenini ambazo zote ametuachia somo la kujifunza.
Kwa miaka zaidi ya sita, Kaseja hakuwa katika kikosi cha Taifa Stars, nafasi ambayo walikuwa wakicheza makipa wengine katika mashindano yote ambayo timu ilikuwa ikishiriki hata zile mechi za kirafiki.
Kaseja alipotea katika soka la Tanzania baada ya kucheza kwa mafanikio Simba, Yanga na Taifa Stars jambo ambalo mashabiki wengi wa soka nchini walifikia hatua ya kumstaafisha na hata kumuita mzee na anatakiwa kuachana na maisha yenyewe ya soka.
Ukomavu ambao Kaseja alionyesha licha ya kukaa nje msimu mzima, alijiunga na Mbeya City ambayo nayo alicheza msimu mmoja kabla ya kujiunga na Kagera Sugar ambayo nayo aliichezea msimu mmoja kabla ya kujiunga na kikosi cha KMC.
Msimu uliopita katika kikosi cha KMC, Kaseja alicheza mechi 15, kati ya hizo hakuna mchezo ambao timu yake ilipoteza hata mmoja jambo ambalo lilimvutia kocha wake, Ettiene Ndayiragije kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuitumikia timu hiyo, kwani mbali na kucheza lakini kuwa kama kiongozi.
Stars wakiwa wanakwenda kucheza mechi na Kenya, kocha wa muda, Ndayiragije alimjumuisha Kaseja katika kikosi cha wachezaji wake ambao watacheza mechi zote mbili na wakiwa katika maandalizi Aishi Manula aliumia jambo ambalo lilitoa nafasi kwa Kaseja kucheza michezo hiyo.
Mwandishi wa makala haya siku moja akiwa katika harakati za kusaka tonge alipita katika kijiwe kimoja na kukuta baadhi ya mashabiki wakibeza kuitwa ka Kaseja katika kikosi cha Stars, wakidai amezeeka na amecheza mpira muda mrefu, kwa maana hiyo nafasi hiyo ilitakiwa awepo kipa mwingine.
Siyo katika kijiwe hicho tu, bali ni vijiwe vingi vya soka na hata katika mitandao ya kijamii walikuwepo waliobeza uwepo wa Kaseja katika kikosi cha Stars, lakini mechi ya Kenya ya marudiano ilitosha Kaseja kuendelea kutupatia somo la kujifunza kutoka kwake.
Miongoni mwa wachezaji ambao wapo katika Ligi Kuu Bara waliocheza soka zaidi ya miaka 15, tena katika kiwango cha hali ya juu, Kaseja ni miongoni mwao licha ya kukutana na changamoto ya maneno mengi ya kubezwa na hata kuitwa majina mengi.
Katika mechi ya kwanza ambayo ilichezwa hapa Dar es Salaam, Kaseja alianza katika kikosi cha kwanza aliokoa mabao mengi ambayo Kenya wangefunga, alicheza mipira hatarishi ambayo kipindi cha zaidi ya miaka sita wakati hayupo kwenye kikosi cha Stars ilikuwa ni hatarishi kwa makipa waliocheza.
Hata katika mechi ya marudiano alionyesha kwamba anastahili kuendelea kubeba mikoba, kwani aliokoa penati na hatari nyinginezo. Kaseja ameonyesha somo la kujifunza kwa wengine.