Karibu tena Bongo mtaalam Fadlu Davids
Muktasari:
- Kuna baadhi ya mambo uliyoyaacha yamebaki vilevile na mengine yamebadilika hivyo jambo la msingi ni uamuzi uko mikononi mwako wa kudumu kwa muda mrefu au uwahi kuondoka.
BONGO imekupenda mwanetu Fadlu Davids ndiyo maana imekuleta kwa mara ya pili kuja kufundisha bolu baada ya mwaka mmoja tangu ulipoondoka.
Kuna baadhi ya mambo uliyoyaacha yamebaki vilevile na mengine yamebadilika hivyo jambo la msingi ni uamuzi uko mikononi mwako wa kudumu kwa muda mrefu au uwahi kuondoka.
Jambo muhimu ambalo kijiwe kinakukumbusha na nadhani wewe mwenyewe ulikabiliana nalo kipindi kile ni hapa soka lake halina rafiki wala adui wa kudumu.
Hao mashabiki wa timu ulipo watakuwa marafiki zako ikiwa watapata matokeo mazuri, timu itatandaza bolu la uhakika na iwapo utafanikiwa kuwapa raha za kumfunga mtani wao.
Kutowapa angalau kimoja kati ya hivyo ambavyo kijiwe kimekutajia, utajiweka kwenye kitanzi braza na hao watakugeuka dakika sifuri tu tofauti na wanavyokusifu hivi sasa baada ya kujiunga nao.
Na tunakukumbusha hiyo timu uliyopo sasa haina uvumilivu kwa kocha na benchi lake la ufundi hivyo usitegemee utapewa muda na kuvumiliwa kama kipindi ulipokuwa kwa watani zao.
Kwa sasa wanaamini wapo katika kilele cha ubabe nje na ndani ya uwanja. Wanaamini wana kikosi kizuri na wana fedha inayowawezesha kuhudumia timu vizuri.
Hawaamini wanatakiwa kufanya vibaya au kutazama mechi kwa presha wakati hayo mambo mawili ya msingi hapo juu wanayo kwenye timu yao ndio maana ni rahisi kwao kutimua kocha.
Msamiati wa projekti kwao watauelewa ikiwa timu itafanya vizuri lakini ikiwa kinyume watakuambia projekti ni Ulaya sio hapa bongo Darisalama.