Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Karia: FVS imetuondolea uhasama kwenye ligi

Muktasari:

  • Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karia amesema kuwa FVS imeonyesha mafanikio makubwa na imesaidia ligi kutokuwa na malalamiko.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kwamba uwepo wa teknolojia ya video ya kusaidia marefa (FVS) imesaidia kupunguza uhasama kwa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) unaofanyika leo Jumamosi, Novemba 14, 2026 jijini Dodoma, Karia amesema kuwa FVS imeonyesha mafanikio makubwa na imesaidia ligi kutokuwa na malalamiko.

“Sasa hivi tunavyoongea mbali na changamoto zilizotokea lakini ndio ligi pekee duniani ambayo inatumia FVS na ligi yetu imekuwa mfano. Na tunapotumia huu mfumo, mechi 150 tunazitolea ripoti.

“Kutumia teknolojia hii kumetusaidia. Tumekutana hapa tuna amani kubwa na kusingekuwa na teknolojia hii pengine tungekuwa tumenuniana hapa.  Uamuzi huu wa kutumia FVS umewezesha waamuzi wetu kuchezesha kwa haki lakini pia kuongeza uadilifu wa ligi yetu lakini tusibweteke, tufanye mambo ambayo yanaendana,” amesema Karia.


KISWAHILI CAF

Karia amefichua kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) liko mbioni kupitisha Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi za shirikisho hilo.

“Mimi binafsi nimewasilisha hoja ambayo imeshapitishwa na kamati ya utendaji ya CAF ya kuomba rasmi Mkutano Mkuu wa CAF upitishe rasmi hoja kwamba lugha ya Kiswahili iwe miongoni mwa lugha rasmi za CAF.

“Ni matarajio yetu kwamba Mkutano Mkuu utakaofanyika Abuja Novemba 21, utapitisha rasmi Kiswahili kuwa moja kati ya lugha rasmi za CAF,” amesema Karia.


AZITAMANI SIMBA, YANGA FAINALI AFRIKA

Karia amesema anatamani Simba na Yanga zikutane katika hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu pia Azam FC na Singida Black Stars kukutana katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Natamani Ligi ya Mabingwa tucheze fainali wenyewe. Natamani Kombe la Shirikisho tucheze wenyewe. Utashi mkubwa zaidi ni angalau mwaka huu kombe moja liweze kubaki hapa,” amesema Karia.


MATUMAINI BENJAMIN MKAPA KUTUMIKA

Karia amesema kwamba ana imani Uwanja wa Benjamin Mkapa utaanza kutumika tena mwezi Januaria 2027.

“Kwa kasi inayoenda, baada ya Januari, naamini tutatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa,” aemsema Karia.

Karia amesema kwamba baada ya fainali za AFCON 2027, ana matumaini viwanja vya mazoezi vitatumika kwa mashindano ya shule Afrika.

“Nia yangu mimi vile viwanja vya Arusha vinavyojengwa na serikali kwa vile vitakuwa na majukwaa, nitashauriana na serikali vitumike kwa ajili ya mashindano ya shule Afrika.

“Nishukuru serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwekeza katika viwanja vya soka,” amesema Karia.


TFF NA UWEKEZAJI WA KLABU

Karia amesema kwamba TFF imeagizwa na FIFA kutengeneza miongozo ya uwekezaji katika klabu za soka.

“Sisi tutaendelea kutengeneza kanuni ambazo pia tutazipitisha kwenu. FIFA imetoa miongozo ya uwekezaji lakini sisi tumetakiwa kutengeneza kanuni na sisi tumeanzisha timu ya wataalam kwa ajili ya kutengeneza hilo.

“FIFA ilituagiza, tengenezeni kanuni ambazo zitasababisha mpira wa miguu ulindwe. Kwa hiyo tunatengeneza miongozo ambayo itatusaidia sisi. Nichukue nafasi hii niwahakikishie kuwa michakato hiyo ambayo sisi tumepewa kuisimamia itaenda kwa haki na hakuna ambaye ataonewa,” amesema Karia.